Bundesliga uwanjani
27 Oktoba 2012Bayern Munich inashikilia uongozi kwa points tano katika Bundesliga na wanaikaribisha Bayer Leverkusen katika uwanja wa Allianz Arena kesho Jumapili, wakati Schalke 04 iko nyuma ya viongozi hao kwa points saba, na Dortmund ambayo inashikilia nafasi ya nne katika msimamo wa ligi iko points 12 nyuma ya viongozi hao.
Bayern ilipata ushindi wa bao 1-0 katika kinyang'anyiro cha Champions League dhidi ya Lille ya Ufaransa siku ya Jumanne, na kulazimisha timu tatu katika kundi la F kuwa na points sita kila mmoja , pamoja na Valencia na BATE Borisov.
Lakini Bayern imeanza vizuri msimu huu wa Bundesliga na wanawania ushindi wao wa mchezo wa tisa mfululizo katika Bundesliga , baada kuvunja rekodi ya kushinda michezo saba baada ya kuiangusha Fortuna Dusselsdorf Jumamosi iliyopita.
Hamasa Dortmund
Mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund wana miadi na Freiburg leo Jumamosi (27.10.2012) wakitiwa hamasa na ushindi wao mnono wa mabao 2-1 dhidi ya Real Madrid, siku ya Jumatano.
Borussia wamefuta majonzi ya kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na watani wao wa jadi Schalke 04 mwishoni mwa juma lililopita, wakati mlinzi wa timu ya taifa ya ujerumani Marcel Schmelzer alipopachika bao la ushindi katika dakika ya 64 na kuwaondoa Rela katika uongozi wa kundi D la champions League.
Schalke 04 iko nyumbani dhidi ya Nuremberg ambayo inashikilia nafasi ya 15. Schalke inaogelea katika furaha ya ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal London.
"Baada ya ushindi katika mchezo wa watani wa jadi wa bonde la Ruhr, ushindi dhidi ya Arsenal ulikuwa ni furaha mara mbili , na najisikia fahari kuwa katika kokosi hiki", amesema mchezaji wa kati wa Schalke na nahidha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21 Lewis Holtby.
Eintracht Frankfurt inayoshikilia nafasi ya pili inaendelea kuwa timu inayoshtua na kutisha msimu huu , baada ya kupata ushindi mara sita katika michezo nane iliyocheza na kesho Jumapili inawania kuendeleza ubabe wake dhidi ya Stuttgart, ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Hamburg wiki iliyopita.
Mwishoni mwa msimamo wa ligi , VFL Wolfsburg inaikaribisha Fortuna Dusseldorf leo jioni , ikiwa chini ya uongozi wa kocha mlenzi Lorenz-Guenther Koestner baada ya klabu hiyo kuvunja ndoa na kocha wa zamani Felix Magath siku ya Alhamis.
Wolfsburg imethibitisha kuwa Magath , mwenye umri wa miaka 59, ambaye alikuwa kocha na meneja wa timu, amejiuzulu baada ya kuwapo kazini kwa siku 586, akiiongoza timu hiyo kama kocha na imepata points tano tu msimu huu na ushindi mmoja tu katika michezo minane, ikiwa ni mwanzo mbaya kabisa kuwahi kutokea katika ligi ya Ujerumani.
Na katika Premier League nchini Uingereza,
Mchezaji wa kiungo wa Manchester United Shinji Kagawa hataonekana uwanjani kwa muda wa wiki nne baada ya kupata maumivu ya goti, wakati wa mchezo wa Champions Legue dhidi ya Braga ya Ureno katikati ya wiki.
Manchester United inakwaana kesho Jumapili na Chelsea, Everton inaonyeshana kazi katika pambano la watani wa jadi na Liverpool, wakati jioni ya leo Arsenal ina miadi na Queens Park Rangers, Manchester City inakwaana na Swansea City.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman