CHADEMA yamjibu Lissu, makada wake kuhusu madai ya rushwa
15 Novemba 2024Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Alhamisi jioni, CHADEMA imesema haijawahi kuletewa hoja ya kugawana majimbo au nafasi za madaraka kutoka kwa serikali.
Ama kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya rasIlimali fedha na rushwa ndani ya chama, CHADEMA imesema inamwalika mtu yeyote mwenye ushahidi au vielelezo vinavyotosheleza, kuwezesha kuchukua hatua za kinidhamu
Taarifa hii inatolewa wakati Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, upande wa Tanzania Bara,Tundu Lissu, amekuwa akiibua hoja kukihusu chama hicho katika mikutano yake anayofanya na wanahabari.
Moja ya hoja ambayo Lissu amekuwa akiibua ni pamoja na kuwa chama hicho kilidanganywa kuhusu suala la maridhiano kwa kuahidiwa baadhi ya nafasi za uongozi ikiwamo ya Uwaziri Mkuu na Makamu wa Rais.Chadema yasema afisa wake mkuu alitekwa na kuumizwa vibaya
Mnamo Mei mwaka huu Lissu akiwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mkoani Iringa, alisema upo mtafaruku mkubwa wa uchaguzi ndani ya chama.
"Msiwe wakali sana mtapewa serikali ya nusu mkate, serikali ya umoja wa kitaifa, baadhi yenu mtakuwa mawaziri, wengine mawaziri wakuu labda." alisema Lissu.
Wachambuzi na makada wa zamani CHADEMA watia neno mtifuano uliopo
Akizungumzia sarakasi hizo ndani ya CHADEMA zinazoua sintofahamu, Mchambuzi wa Masuala ya siasa kutoka Shule ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Profesa Ibrahim Bakari amesema ishara hiyo si nzuri kwa vyama vya upinzani.Polisi yamtia mbaroni kiongozi maarufu wa upinzani Tanzania
"Migogoro ni jambo la kawaida, lakini inapotokea katika kipindi hiki, inatakiwa iangaliwe kwa umakini zaidi, kwa ujenzi wa chama kama taasisi, hizi kauli za kupishana pishana viongozi kuhusiana na mwelekeo wa chama sio jambo zuri hasa katika kipindi hiki"
Pamoja na Lissu, aliyekuwa kiongozi wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa amewahi kunukuliwa akisema, anachukizwa na jinsi CHADEMA kinavyokaa kimya kuhusu tuhuma anazotoa Lissu.
DW imefanya mazungumzo na Dk Slaa baada ya CHADEMA kutoa taarifa yake na alikuwa na haya ya kusema:
"Masuala ya rushwa usipoyasema lazima taifa linaangamia, CHADEMA itaangamia, taifa zima litaangamia... Mimi niseme kitendo hicho nimekifurahia, na Lisu niemfanya kazi naye namfahamu Lissu hamumunyi maneno pale ambapo anataka kusema jambo ambalo linaumiza taifa lake"
Hii sio mara ya kwanza kwa CHADEMA kujiba tuhuma zinazoibuliwa na makada wake, Agosti 17 mwaka huu CHADEMA kilijibu hoja za Lissu alizozitoa akikitaka chama kijibu tuhuma za ufisadi unaoibuliwa na aliyekuwa mwanachama wake, Mchungaji Peter Msigwa tangu alipohamia CCM, Juni 30 mwaka huu.