Chama tawala Burundi kimeishutumu Rwanda
28 Machi 2016Katika taarifa ambayo shirika la habari la Ufaransa AFP liliipata hapo jana, mkuu wa chama cha CNDD-FDD amesema awali Kagame alifanya jaribio la mauwaji ya kimbari akimaanisha mauwaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994, ambapo kiasi ya watu 800,000 waliuwawa wengi wao kutoka jamii ya kabila la Watutsi.
Katika maandiko yake hayo rais wa CNDD-FDD Pascal Nyabenda amesema maabara ya mauwaji ya halaiki yapo Rwanda kwa sababu rais Kagame amekuwa na majaribio huko na kutaka kuyaingiza Burundi akifanya ubeberu mdogo.
Kuzorota kwa mahusiano
Mahusiano kati ya mataifa hayo ya Kanda ya Maziwa Makuu yapo katika kiwango cha chini sana, huku Burundi na Umoja wa Mataifa wakiituhumu Rwanda kuunga mkono waasi wa Burundi. Nyabenda vilevile alidai baadhi ya mataifa ya Ulaya yanatoa silaha na fedha kwa kiongozi wa Rwanda, ambayo anasema inawajibika na kusajili na kuwafunza vijana wa Kirundi, katika kambi za wakimbizi nchini Rwanda, ili waweze kurejea nyumbani kufanya vitendo vya mauwaji ya halaiki.
Mkuu huyo wa chama alienda mbali zaidi na kulikosoa kanisa Katoliki ambalo hivi karibuni lilitoa wito wa kufanyika mazungumzo baina ya serikali ya Burundi na Rwanda ili kuepusha kueneza zaidi kwa mgogoro huo unaonendelea kukuwa.
Nyibenda vilevile alilaani waandishi wa habari wa kigeni kwa kuchua mkondo wa taarifa za wale aliowaita "magaidi" jina ambalo chama tawala kinatumia kuwaita wapinzani wao wote wale wenye silaha na wa amani.
Burundi iliingia katika mgogoro wa kisiasa tangu Aprili mwaka uliopita, pale ambapo Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kwa utata kuwania muhula wa tatu, ambayo ilifanikisha ushindi wake katika uchaguzi wa Julai.
Baadae kulitokea machafuko ambayo yalisababisha watu 400 kupoteza maisha, huku wengine 250,000 wakilikimbia taifa hilo na kwamba mashambulizi yameendelea kutokea kila siku, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa hofu ya kurejea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kama vile vya 1993-2006.
Chama tawala cha CNDD-FDD kiliundwa na kundi kuwa la waasi kutoka kabila la Wahutu, ambao walikuwa wakikabiliana na kile kilichofahamika kuwa jamii ya wachache ya Watutsi walikuwa wamelidhibiti jeshi wakati wa vita vya wenyew kwa wenyew vya Burundi.
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri:Iddi Ssessanga