Senegal:Pastef yadai kupata ushindi katika uchaguzi wa Bunge
18 Novemba 2024Chama cha Pastef chake Rais Bassirou Diomaye Faye, kilikuwa kikisaka wingi wa kutosha bungeni, ili kumuwezesha Faye kutekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyaahidi, ikiwa ni miezi minane tangu alipoingia madarakani.
Wapigakura zaidi ya milioni saba waliwachagua wabunge 165 watakaohudumu kwa kipindi cha miaka mitano. Bunge lilikuwa likiongozwa na upinzani na lilitatiza shughuli za serikali, jambo ambalo lilimfanya Faye kulivunja bunge mwezi Septemba na kuitisha uchaguzi wa mapema mara tu katiba ilipomruhusu kufanya hivyo.
Akiwa nje ya nchi, rais wa zamani Macky Sall anaongoza kundi la upinzani liitwalo Takku Wallu Senegal. Hapo jana, alidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kile alichokiita "udanganyifu mkubwa ulioandaliwa na chama cha Pastef", bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.