Colombia na waasi wa FARC wafikia makubaliano mapya
13 Novemba 2016Makubaliano hayo yanakuja wiki sita baada ya makubaliano ya awali kukataliwa katika kura ya maoni kutokana na madai kwamba makubaliano hayo yalikuwa yanawapendelea mno waasi.
Serikali na waasi wa kundi la Revolutionary Armed Forces , majeshi ya kimapinduzi ya Colombia, FARC , ambao wamekuwa wakifanya mazungumzo mjini Havana kwa muda wa miaka minne, wamesema wamejumuisha mapendekezo kutoka kwa upinzani, viongozi wa kidini na wengine.
Rais Juan Manuel Santos ana matumaini ya kuliunganisha taifa hilo lililogawika kwa kutumia makubaliano hayo mapya baada ya hatua za amani kuhatarishwa na wananchi kukataa katika kura ya maoni mwezi Oktoba. Wapiga kura wa Colombia waligawanyika kwa kiasi kikubwa , wengi wao wakiwa na wasi wasi wasi kwamba waasi wa FARC hawataadhibiwa kwa uhalifu na wengine wakiwa na matumaini kwamba makubaliano hayo yataimarisha kumalizika kwa machafuko na ghasia.
"Tunatoa wito kwa Wakolombia wote na jumuiya ya kimataifa kuunga mkono makubaliano haya mapya na utekelezaji wake wa haraka ili kuweza kutupilia mbali maafa ya vita," pande hizo mbili zilisema katika taarifa. "Amani haiwezi kusubiri tena." Nakala za makubaliano hayo mapya zitasambazwa kwa umma kuanzia leo Jumapili(13.11.2016).
Serikali haijasema iwapo itafanya kura nyingine ya maoni kuidhinisha makubaliano hayo, licha ya kuwa baadhi ya viongozi wa upinzani tayari wanadai kufanyika kwa kura hiyo kupitia ukurasa wa Twitter.
Makubaliano hayo mapya hayajabadilisha sehemu tata ya makubaliano hayo ambayo yanatoa kwa kundi la FARC viti 10 katika bunge la nchi hiyo hadi mwaka 2026 ama kuwazuwia viongozi wa waasi kuchaguliwa katika nyadhifa za kisiasa.
Makubaliano hayataingizwa katika katiba
Hata hivyo , makubaliano hayo hayataingizwa katika katiba ya Colombia na kundi la FARC litatakiwa kuwasilisha orodha ya vifaa vyake vyote na mali, ambavyo vitatumika kwa madhumuni ya kuwalipa fidia waathirika, Santos alisema katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni.
Makubaliano hayo yaliyofanyiwa mabadiliko pia yanaondoa majaji wa kigeni katika mahakama maalum za amani , licha ya kwamba kutakuwa na wachunguzi wa kigeni, na kueleza kwamba FARC ni lazima kutoa taarifa za kina juu ya kuhusika kwao katika biashara ya mihadarati.
Makubaliano hayo mapya yanaweka ukomo katika kazi ya mahakama maalum hadi miaka 10 na yanataka uchunguzi wowote kufunguliwa katika muda wa miaka miwili ya mwanzo.
Wasi wasi mkubwa miongoni mwa wale waliopiga kura ya "hapana" katika makubaliano ya awali ni kwamba waasi waliohukumiwa hawatatumikia kifungo chao jela na badala yake watafanya kazi ya kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini na kufanya kazi nyingine.
Haionekani kuwa mabadiliko yatajumuisha kifungo cha jela, lakini Santos amesema makubaliano hayo yatahakikisha wapiganaji wa FARC waliohukumiwa na mahakama maalum watazuiliwa katika maeneo maalum, wakifanyakazi na utaratibu mwingine.
Wazo la upinzani
Wazo la upinzani kwamba viongozi wa FARC wasiruhusiwe kugombea nyadhifa za kisiasa mara watakapomaliza kifungo chao halikujadiliwa pamoja na waasi, Santos alisema. "Hatua tulizochukua pamoja na FARC sio na haziwezi kuwa za aina yake."
Rais wa zamani Alvaro Uribe , ambae aliongoza upande wa upinzani katika makubaliano ya awali, hajafurahishwa na makubaliano hayo yaliyofanyiwa mabadiliko, vyanzo vimesema. Uribe ambaye alikutana na Santos , jana Jumamosi, alisema kambi yake na waathirika wanapaswa kupitia makubaliano hayo mapya kabla ya utekelezaji.
"Nimemuomba rais kwamba chapisho la makubaliano lililotangazwa Havana halipaswi kuwa la mwisho," amesema katika taarifa, na kuongeza kwamba upinzani huenda ukahitaji kufanya mapendekezo zaidi. Santos alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwezi uliopita kwa juhudi zake za kumaliza vita hivyo, ambavyo vimesababisha watu zaidi ya 220,000 kuuwawa na wengine wengi kukimbia makaazi yao.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi