Mtandao wa intaneti na simu vyafungiwa
1 Desemba 2016Gambia imefunga mtandao wa intaneti na simu katika taifa hilo dogo la Afrika magharibi leo, wakati upigaji kura katika uchaguzi wa rais ukianza nchini humo.
Kufungwa kwa mitandao na mawasiliano ya simu , na watoaji huduma za intaneti ambako kunayaathiri makampuni yanayomilikiwa na serikali na pia makampuni ya binafsi, kunakuja wakati utawala wa rais Yahya Jammeh wa miaka 22 unakabiliwa na upinzani mkubwa kwa mara ya kwanza.
Kanali huyo wa zamani wa jeshi, ambaye aliingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1994 na analitawala taifa hilo kwa mkono wa chuma, anawania kipindi cha tano dhidi ya wagombea wengine wawili.
Mpizani wake mkubwa Adama Barrow, anaungwa mkono na vyama saba vya upinzani na ni maarufu akikubalika na vijana wengi wa nchi hiyo ambao hawana ajira. Mfanyabiashara huyo anaahidi kurejesha demokrasia na utawala wa sheria na kuwaacha huru wafungwa wote wa kisiasa.