Juan Guaido asema hatua za Maduro hazimtishi
1 Februari 2019Hatua hiyo imeongeza hofu ya usalama kwa kiongozi huyo wa upinzani Juan Guaido aliye na miaka 35, aliyejitangaza kuwa rais wa mpito wiki iliyopita, katika hatua ya kijasiri ya kuupinga utawala wa Nicolas Maduro.
Akizungumza katika chuo kikuu cha Caracas, Guaido alisema kikosi hicho maalumu cha jeshi la polisi kilikwenda nyumbani kwake kumhoji mkewe Fabiana Rosales Guaido.
Juan Guaido ameonya kuwa maafisa hao wa usalama watawajibishwa iwapo familia yake itadhurika, na kwamba kwa sasa hawatishiki.
Hata hivyo polisi imekanusha kuhusika na tukio hilo kwa kuandika katika mtandao wake wa twitter kwamba taarifa zinazotolewa na Guaido hazina ukweli wowote.
Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amesema dunia inaangalia kinachoendelea Venezuela na Marekani haitovumilia hatua zozote za kuwadhuru wale wanaopigania uhuru na demokrasia ya Venezuela.
Juan Guaido ajaribu kuwashawishi China na Urusi wamuunge mkono
Dunia imeendelea kugawika kati ya mataifa yanayomtaka Nicolas Maduro kuendelea kuwepo madarakani na wale wanaomshinikiza ajiuzulu huku Guaido akiendelea kujaribu kuwafikia adui zake China na Urusi.
Guaido ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ametuma barua kwa nchi zote mbili ambazo ni wakopeshaji wakuu wa kigeni wa Venezuela na wanaomuunga mkono Maduro katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya wasiwasi wa taifa hilo kutolipa deni lake.
Guaido amesema litakuwa jambo jema iwapo Urusi na China zitamuunga mkono na kubadilisha mkondo wao kwa Venezuela ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi OPEC. Awali wabunge wa ulaya walimtambua Guaido kama kaimu rais wa Venezuela ikiwa ni hatua moja mbele ya kumng'oa madarakani kiongozi wa kisoshalisti alioudidimiza uchumi wa Venezuela.
Mataifa manne yalioyo na nguvu barani Ulaya Uingereza Ufaransa Ujerumani na Uhispania zimesema zitamtambua Juan Guaido iwapo rais Maduro atatangaza uchaguzi mwishoni mwa juma huku Maduro mwenyewe akisema uchaguzi utakaokuwepo ni ule wa mwaka 2025.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mahriri: Josephat Charo