Guteress awatolea wito viongozi wa G20 kuhusu COP29
18 Novemba 2024Antonio Guterres amewatolea wito viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani wa G20 waliokusanyika nchini Brazil, kufanikisha mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa ya COP29 yanayoendelea nchini Azerbaijan.
Guterres, ambaye atahudhuria mkutano wa kilele wa G20 unaoanza hivi leo huko Rio de Janeiro, amesema matokeo yenye mafanikio katika COP29 bado yanaweza kufikiwa, lakini yatahitaji uongozi na maelewano kutoka kwa nchi za G20.
Soma pia: G20 yahimizwa kutanzua mkwamo wa mazungumzo ya COP29
Mazungumzo ya COP29 mjini Baku yamekwama licha ya wiki moja ya majadiliano, huku mataifa yakishindwa kuafikiana mkataba wa dola trilioni 1 kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya hali ya hewa katika mataifa yanayoendelea.
Mbali na kiwango hicho, bado kuna mivutano pia kuhusu aina ya ufadhili na nani anayepaswa kutoa fedha hizo, huku nchi za Magharibi zikiitaka China na mataifa tajiri ya Ghuba kujiunga katika orodha ya wafadhili.