Guterres alaani vurugu za Senegal
3 Juni 2023Kauli hiyo ameitoa baada ya vurugu zilizotokana na kufungwa kwa kiongozi wa upinzani ambazo zimesababisha watu tisa kupoteza maisha.
Naibu Msemaji wa Guterres, Farhan Haq aliwaambia waandishi wa habari kwamba katibu mkuu huyo ametoa salamu za pole kwa wale wote waliowapoteza ndugu zao katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Soma zaidi:Watu 9 wauawa kwa maandamano ya kupinga hukumu ya Sonko
Wito kama huo umetolewa na Umoja wa Afrika ambapo rais wa kamisheni ya umoja huo, Moussa Faki Mahamat, alilaani vikali ghasia hizo na kuwataka viongozi kuepuka vitendo vinavyoharibu sura ya demokrasia ya Senegal, ambayo Afrika imekuwa ikijivunia.
Maandamano yalizuka baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela Alhamisi, kwa kuwalaghai vijana hatua ambayo wafuasi wake wanasema imebuniwa kisiasa ili wamzuie kugombea uchaguzi wa mwakani.